NA EMMANUEL MBATILO, DODOMA

Wizara ya Viwanda na Biashara kupitia Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (TIRDO) imeendelea kuimarisha sekta ya viwanda nchini kwa kufanya tathmini ya viwanda, kuboresha maabara za kisasa pamoja na kuendeleza teknolojia za uzalishaji zinazolenga kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Akizungumza leo Mei 22, 2026 bungeni jijini Dodoma wakati akiwasilisha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga amesema TIRDO imeendelea kutekeleza zoezi la tathmini ya viwanda na kubaini fursa za uwekezaji katika maeneo mbalimbali nchini.

Amesema tathmini hiyo inalenga kubaini idadi ya viwanda, ajira, uwezo wa uzalishaji, teknolojia zinazotumika pamoja na maeneo yenye fursa za uwekezaji ili kuchochea maendeleo ya viwanda na kuongeza thamani ya rasilimali za ndani.

Kwa mujibu wa Kapinga, zoezi hilo limefanyika katika mikoa miwili mipya na kufanya jumla ya mikoa iliyofikiwa kufikia tisa ambayo ni Pwani, Morogoro, Dar es Salaam, Kilimanjaro, Tanga, Arusha, Manyara, Mwanza na Shinyanga.

Aidha, amesema taarifa zote zilizokusanywa zimeingizwa katika mfumo wa kanzidata za viwanda ambapo hadi Aprili 2026 kulikuwa na jumla ya viwanda 25,650 vilivyosajiliwa.

“Kati ya viwanda hivyo, 482 ni vikubwa, 625 vya kati, 8,980 vidogo na 15,563 ni viwanda vidogo sana,” amesema Kapinga.

Katika hatua nyingine, Waziri huyo amesema TIRDO imeendelea kuimarisha maabara zake kwa ajili ya utoaji wa huduma za kitafiti katika maendeleo ya viwanda.

Ameeleza kuwa maabara ya chakula iliyopata ithibati mwaka 2025 imeboreshwa kwa kuongeza huduma kutoka tatu hadi sita pamoja na kuongeza wigo wa bidhaa kutoka moja hadi nne.

Bidhaa hizo ni pamoja na vyakula vilivyotayari kwa matumizi, nyama na bidhaa zake, samaki na bidhaa zake pamoja na sampuli za usufi wa nyuso.

Kapinga amesema hatua hiyo itaongeza uwezo wa maabara kutoa huduma za kuaminika zaidi huku ikipunguza utegemezi wa huduma kutoka nje ya nchi.

Pia amesema TIRDO inaendelea na jitihada za kuanzisha Maabara ya Nishati na Madini katika Mkoa wa Njombe ili kusogeza huduma karibu na maeneo yenye shughuli za uzalishaji na rasilimali za madini.

Amesema maabara hiyo itahudumia mikoa ya Nyanda za Juu Kusini ikiwemo Ruvuma, Mbeya na Rukwa, huku ikitarajiwa kufanya vipimo vya ubora wa makaa ya mawe, kemikali, madini pamoja na nishati mbadala ikiwemo biomasi na mkaa mbadala.

“Hadi Aprili 2026, Shirika limefanikiwa kumpata mzabuni wa kusambaza na kusimika vifaa vya kisasa pamoja na kutoa mafunzo kwa wataalam watakaoendesha maabara hiyo,” amesema.

Kapinga aliongeza kuwa kukamilika kwa maabara hiyo kutachochea uchumi wa viwanda unaozingatia nishati safi na rafiki kwa mazingira.

Sambamba na hayo, amesema TIRDO inaendelea na mchakato wa kupata ithibati kwa maabara zake za mazingira, kemia, makaa ya mawe, mafuta na gesi ili kuongeza ubora wa huduma zinazotolewa.

Katika eneo la ubunifu na teknolojia, Waziri Kapinga alisema Wizara kupitia Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) imefanikiwa kuhawilisha teknolojia nane za uchakataji wa mazao na uzalishaji.

Teknolojia hizo ni pamoja na mashine za kutengeneza mkaa mbadala, kusafisha mafuta ya alizeti, kuzalisha chakula cha samaki, kubangua korosho, kukamua mafuta ya nazi pamoja na mashine za kusaga mawe yenye madini.

Aidha, amesema SIDO kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda la Umoja wa Mataifa (UNIDO) imetengeneza mashine tatu za kuzalisha mkaa mbadala na kuanzisha teknolojia mpya kutoka Japan katika maeneo ya Ifakara, Kahama na Mwanjelwa.

Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: