
Na Oscar Assenga, Lushoto
Mkuu wa Wilaya ya Lushoto, Zephania Sumaye, ameishukuru Benki ya NMB Bank Plc kwa kuandaa tukio la kipekee la Kijiji Day, akisema ni hatua muhimu katika kuwafikia wananchi vijijini na kuwapatia elimu ya kifedha.

Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa TAMISEMI, Prof. Riziki Shemdoe ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Lushoto (CCM), alisema kuwa wizara ina malengo mahsusi ya miaka mitano, likiwemo kuhakikisha wananchi wanapata uhuru wa kiuchumi.
Alisisitiza kuwa uhuru huo hauwezi kupatikana bila wananchi kujihusisha na taasisi za kifedha, ikiwemo benki kama NMB.

Alieleza kuwa tukio la Kijiji Day ni sehemu ya utekelezaji wa malengo hayo, kwani linawawezesha wananchi kupata elimu ya kifedha pamoja na huduma mbalimbali za kibenki moja kwa moja walipo.
Tukio hilo lilifanyika katika Kata ya Magamba, ambapo wananchi walipata fursa ya kujifunza na kunufaika na huduma zinazotolewa na benki hiyo.
Aidha, alisema moja ya malengo ya serikali ni kuhakikisha jamii ya Lushoto inaunganishwa na kuwa kitu kimoja.

Alibainisha kuwa njia mojawapo ya kuimarisha mshikamano huo ni kupitia michezo na mabonanza, kama ilivyofanyika katika tukio hilo ambapo NMB ilitumia siku nzima kushirikiana na wananchi wa Kijiji cha Magamba.
Alisisitiza umuhimu wa elimu kwa maendeleo ya mwanadamu, akieleza kuwa hata katika mafundisho ya dini mbalimbali, elimu imepewa kipaumbele kikubwa.
Alifananisha juhudi za NMB na msemo usemao: “Usimpe mtu samaki, mfundishe kuvua.” Akasema benki hiyo inafanya kazi kubwa kwa kuwafundisha wananchi namna ya kutumia huduma za kifedha kwa ufanisi, badala ya kuwapatia msaada wa moja kwa moja bila uelewa.

Aliongeza kuwa kama benki zingetoa mikopo bila elimu ya matumizi sahihi, matokeo yasingekuwa endelevu,Hivyo, matukio kama Kijiji Day yanafungua njia ya kuwafikia wananchi, kuwapa elimu na kuwasogezea huduma za kifedha karibu zaidi.
Aliwahimiza NMB kuendelea na juhudi hizo pamoja na kuandaa mabonanza yatakayoongeza furaha, mshikamano na uelewa wa wananchi kuhusu huduma zao, jambo litakalosaidia kujenga imani na umiliki wa wananchi kwa benki hiyo.
Katika tukio hilo la Kijiji Day lililofanyika Magamba, shughuli mbalimbali zilifanyika ikiwemo mbio za marathon, huduma ya chakula, pamoja na mabonanza mengine. Lengo kuu lilikuwa ni kuwafikia wananchi, kuwapa elimu ya kifedha na kuwajengea uelewa mpana kuhusu huduma za benki.
Awali akizungumza Meneja wa Kanda ya Kaskazini wa NMB Bank Plc, Baraka Ladislaus, amesema benki hiyo inaendelea kusogeza huduma za kifedha karibu na wananchi kupitia matamasha ya Kijiji Day yanayofanyika vijijini.
Alisema lengo la mpango huo ni kuwafikia wananchi walipo, kuwapatia elimu ya kifedha na kuwaunganisha na huduma mbalimbali za kibenki ili kuwawezesha kiuchumi.

Alieleza kuwa pamoja na elimu ya kifedha, tukio hilo linaambatana na shughuli za kijamii ikiwemo upandaji miti kwa kushirikiana na Taifa Gas, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuhifadhi mazingira na kuifanya Tanzania kuwa ya kijani.

Aidha, alisema NMB ina mtandao mpana wa mawakala zaidi ya 80,000 nchi nzima wanaotoa huduma karibu asilimia 60 ya mahitaji ya kifedha ya wananchi, sambamba na matumizi ya magari maalum ya kibenki yanayowafikia wananchi vijijini.

Aliongeza kuwa benki hiyo imeboresha huduma zake za kidijitali ikiwemo programu ya NMB Mkononi, inayorahisisha upatikanaji wa huduma kwa wateja popote walipo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Whitney Mwinzagi aliwataka wananchi kutumia vyema elimu wanayoipata na kuelekeza mikopo wanayoipata kuitumia shughuli za uzalishaji mali badala ya matumizi yasiyo na tija.







Post A Comment: