Baadhi ya wananchi waliotembelea banda la Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) katika Kliniki maalum ya kutatua kero za wananchi iliyofanyika katika viwanja vya Nyerere Square, jijini Dodoma, wameshauri Wakala kuanza kujenga nyumba za makazi kwa ajili ya kupangishwa kwa watu binafsi kutokana na kuongezeka kwa mahitaji ya nyumba za kupanga katika mkoa huo.

Ushauri huo umetolewa wakati wa kliniki hiyo iliyolenga kusikiliza na kutatua changamoto mbalimbali za wananchi, sambamba na kuonesha miradi iliyotekelezwa ndani ya siku 100 za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu kuingia madarakani.

Wananchi hao wamesema kuwa pamoja na mahitaji ya nyumba za makazi kwa watumishi wa umma, bado kuna uhitaji mkubwa wa nyumba za kupanga kwa wananchi wa kawaida wanaoishi katika Jiji la Dodoma.

Bi. Saada Salum, mkazi wa Nzuguni Boda, amesema kuwa upatikanaji wa nyumba za kupanga bado ni changamoto kwa wakazi wengi wa Dodoma, hivyo TBA inapaswa kufikiria kupanua huduma zake ili kuwahusisha pia watu binafsi.

“Suala la nyumba za kupanga hapa Dodoma ni changamoto. Watu wengi wanahitaji nyumba za kupanga. TBA mnatakiwa kufikiria sasa kuanza kujenga nyumba na kupangisha watu binafsi ili nao waweze kukaa kwenye nyumba zenu, si watumishi wa serikali pekee yao,” amesema Bi. Salum.

Kwa upande wake, Peter Masule, mkazi wa Nzuguni kwa Masista, ameishukuru TBA kwa kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 3,500 katika eneo hilo, akisema kuwa mradi huo umechangia kuimarika kwa hali ya usalama tofauti na ilivyokuwa awali.

Amesema kabla ya mradi huo kulikuwa na matukio mengi ya uhalifu katika eneo hilo, ambapo wahalifu walikuwa wakitumia vichaka vilivyokuwepo kujificha baada ya kufanya wizi.

“Mimi nimekuwa mkazi wa Nzuguni kwa muda mrefu. Kabla ya mradi wa nyumba hizi kulikuwa na matukio mengi ya uhalifu, vibaka walikuwa wakija kujificha kwenye vichaka baada ya kufanya wizi. Lakini sasa matukio hayo yamepungua sana,” amesema Masule.

Wananchi hao pia wameeleza kuwa uwepo wa mradi wa nyumba hizo umechangia kuboresha mandhari na kupendezesha eneo la Nzuguni.

Kupitia kliniki hiyo, TBA pia imepata fursa ya kukutana na wadau na wateja wake, wengi wao wakiwa ni wapangaji wa nyumba zake, ambapo baadhi ya changamoto walizowasilisha zimepatiwa ufumbuzi papo hapo.

Kliniki hiyo ya siku tatu ilianza Jumatano, Machi 4, 2026 na kuhitimishwa Ijumaa, Machi 6, 2026 katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma.

Share To:

Alex Sonna

Post A Comment: