Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan imeendelea kuleta neema ya maendeleo kwa wananchi wa mkoa wa Arusha kwa kuanza utekelezaji wa mradi wa kusambaza umeme katika vitongoji 127 kwa gharama ya shilingi bilioni 19.5.
Mradi huo unatekelezwa kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika awamu ya Pili B na unatarajiwa kuwanufaisha wateja 4,086 katika wilaya za Arusha DC, Meru, Karatu, Ngorongoro, Longido na Monduli.
Akizungumza Februari 4, 2026 mkoani Arusha wakati wa hafla ya kumtambulisha mkandarasi aliyeshinda zabuni, Mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Herini Mhina, amesema utekelezaji wa mradi huo ulianza rasmi Februari 2, 2026 na mkandarasi mzawa Kampuni ya NAKUROI Investment Co. Ltd.
“Tunamshukuru Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia utekelezaji wa mradi huu muhimu. Tumewaelekeza wakandarasi kuepuka rushwa, kutumia vibarua wa maeneo husika kwa kazi zisizo za kitaalamu na kuhakikisha mradi unatekelezwa kwa ubora na kwa wakati,” amesema Mhandisi Mhina.
Mhandisi Mhina ameongeza kuwa hadi sasa vitongoji 368 kati ya 1,505 mkoani Arusha vimefikishiwa umeme, huku jitihada zikiendelea kufikisha nishati hiyo katika vitongoji vilivyobaki.
“Dhamira ya Serikali ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2030 vitongoji vyote nchini viwe vimefikishiwa umeme. REA imejipanga kikamilifu kutekeleza dhamira hiyo kupitia miradi mbalimbali ya kimkakati,” amefafanua Mhandisi Mhina.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. CPA Amos Makala, ameipongeza REA kwa kutekeleza kwa vitendo maelekezo na dira ya Rais Samia ya kuwaletea wananchi maendeleo.
“Ofisi ya Mkuu wa Mkoa itatoa ushirikiano wa kutosha kwa mkandarasi na REA kuhakikisha mradi huu unakamilika kwa mafanikio,” amesema Mhe. Makala.
Naye Meneja wa Mradi kutoka Kampuni ya NAKUROI Investment Co. Ltd, Mhandisi Selestine Egongo, ameishukuru Serikali kwa kuwaamini na kuahidi kutekeleza mradi kwa ufanisi kwa kushirikiana na viongozi na wananchi wa maeneo husika.


Post A Comment: