Serikali, kupitia taasisi zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara, imesisitiza kuendelea kuwadhibiti watu wanaoingiza bidhaa duni nchini kupitia njia haramu ikilenga kulinda afya za walaji na uchumi wa Taifa.

Hayo yamesemwa, Aprili 16, 2026, jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Salum, alipofanya ziara katika Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kukagua utendaji kazi wa shirika hilo pamoja na miundombinu ikiwa ni pamoja na maabara 12 za udhiti ubora.

Balozi Waziri ameeleza kuridhishwa na huduma za uhakiki wa ubora zinazotolewa na TBS, huku akiwahakikishia Watanzania kuwa bidhaa zote zilizopita kwenye mikono ya shirika hilo na kupata nembo ya ubora ni salama kwa matumizi.

Amesema kuwa Serikali itaendelea kuhakikisha bidhaa zote zinazozalishwa nchini na zile zinazoingizwa kutoka nje zinafanyiwa uhakiki wa kina, huku akiwasihi wafanyakazi wa TBS kufanya kazi kwa weledi, utu na nidhamu ili kufikia malengo ya taasisi na Taifa kwa ujumla.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, amebainisha kuwa shirika hilo kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), linaendelea kuwawezesha wajasiriamali wadogo kwa kuwapa mafunzo na miongozo ya kitaalamu kuhusu uhakiki wa bidhaa zao.

Aidha, Dkt. Katunzi ameishukuru Serikali ya Rais Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuiwezesha TBS kupata miundombinu ya kisasa na vifaa bora vya maabara vyenye gharama kubwa, hali inayorahisisha utendaji kazi wa shirika hilo.
Share To:

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: