Mgombea wa Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kuimarisha miundombinu ya barabara na kukabiliana na changamoto ya wanyama wakali kuvamia makazi na mashamba ya wananchi wa Mangaka na maeneo jirani.
Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Septemba 23, 2025, mjini Mangaka, wilayani Nanyumbu, Dkt. Samia amesema serikali itahakikisha barabara za lami ndani ya mji huo zinakamilika sambamba na ujenzi wa mitaro ya maji ya mvua kwa ajili ya kulinda miundombinu hiyo.
“Tutafanya kazi ya kuimarisha barabara za lami ndani ya mji wa Mangaka pamoja na mitaro, lakini vile vile tutaendelea kujenga barabara zinazounganisha wilaya na makao makuu ya mkoa wenu, aidha kwa changarawe zipitike mwaka mzima na kama kuna madaraja tutajenga madaraja na nyingine tutakwenda kuzijenga kwa lami,” amesema Dkt. Samia.
Aidha, amehidi kuendelea kushughulikia changamoto kubwa inayowakabili wananchi wa Mangaka na maeneo jirani ya wanyamapori kuvamia makazi na mashamba, hali inayosababisha hofu na hasara kwa wakulima.
Dkt. Samia amesema dhamira ya serikali ni kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na kuendelea na shughuli zao za uzalishaji bila bughudha ya wanyama pori, huku miundombinu bora ya barabara ikiimarisha biashara na maendeleo ya wananchi.

Post A Comment: