Rais wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Dkt. Akinwumi Adesina amepongeza jitihada na maono ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya miundombinu na ya Kimkakati, akiahidi kuwa Benki hiyo itaendelea kuwa Mbia wa Serikali ya Tanzania, katika kufanikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo nchini.

Rais Dkt. Adesina amebainisha hayo wakati wa mkutano wa hadhara wa Rais Samia Mkoani Dodoma leo Jumamosi Juni 14, 2025, muda mfupi mara baada ya Rais Samia kukagua utekelezaji wa ujenzi wa uwanja wa Kimataifa wa ndege Msalato pamoja na ujenzi wa barabara ya mzunguko wa nje wa Jiji la Dodoma yenye urefu wa Kilomita 112.3.

Katika salamu zake, Dkt. Adesina amemtaja Rais Samia kama Kiongozi wa mfano barani Afrika na duniani kote kutokana na namna ambavyo ameendelea kufanikisha maendeleo kwenye sekta mbalimbali nchini sambamba na jitihada zake katika kuimarisha utengamano wa Kikanda.

Dkt. Adesina ambaye Benki yake inafadhili pia ujenzi wa uwanja wa ndege Msalato pamoja na barabara ya Mzunguko Dodoma, ameeeleza kuridhishwa na maendeleo ya ujenzi huo pamoja na mafanikio yaliyopatikana kwenye ujenzi wa reli ya kisasa SGR, akisema Benki hiyo itaendelea kushirikiana na  Tanzania katika kuendeleza shoroba zinazoanzia bandari ya Dar Es salaam na kuunganisha nchi nane zinazoizunguka Tanzania na zisizokuwa  na mlango wa bahari.

Kulingana na Rais huyo wa Benki ya Afrika anayemaliza muda wake, Benki hiyo imetoa zaidi ya Dola bilioni 9 za Marekani kwa Tanzania ambapo katika fedha hizo Dola Bilioni 4.73 zimetolewa katika kipindi chake cha uongozi, akiwa pia ndiye Rais pekee wa Benki hiyo aliyeitembelea na kufanya kazi na Tanzania kwa ukaribu zaidi tangu kuanzishwa kwa benki hiyo mwaka 1971.

Share To:

Post A Comment: