Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka, Juni 12,2024 alifanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Halmashauri ya Mji Njombe na kueleza kuridhishwa na hatua zilizofikiwa kwenye miradi hiyo muhimu ya sekta ya elimu.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mtaka alitembelea ujenzi wa jengo la gorofa lenye vyumba 8 vya madarasa na ofisi 4 za walimu na matundu 4 ya vyoo katika Shule ya Sekondari Uwemba, mradi uliokadiriwa kugharimu zaidi ya shilingi milioni 600 hadi kukamilika.Pia alikagua ujenzi wa shule mpya ya Sekondari Wikichi unaotekelezwa kupitia programu ya SEQUIP kwa gharama ya shilingi milioni 583.
Mhe. Mtaka alitoa pongezi kwa Halmashauri ya Mji Njombe kupitia Mkurugenzi wake Bi.Kuruthum Sadick kwa kutenga fedha za mapato ya ndani ili kuendeleza ujenzi wa jengo hilo la gorofa, pamoja na kusimamia vizuri miradi yote inayotekelezwa. \n\nAidha, alisifu mafundi wanaotekeleza kazi hizo kwa weledi na kujituma kwao kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
"Mkurugenzi umejionea mwenyewe namna mafundi walivyofanya vizuri kuanzia kwenye gorofa, tafuta namna tuwaite pamoja na bodi ya usajili wakandarasi na benki ili waweje kujisajili na tuhakikishe tunaendelea kuwapa kazi maana huu ni uaminifu mkubwa majengo kama haya ni mwanzo mzuri."Alisema Mhe.Mtaka.
Mradi wa ujenzi wa jengo la gorofa katika Shule ya Sekondari Uwemba uliibuliwa na wananchi wa kata ya Uwemba mwaka 2022 kwa kushirikiana na Mhe.Mbunge,Diwani na uongozi wa shule.Mradi huo unatekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu, michango ya wananchi na wadau wa maendeleo, mchango wa Mbunge wa Jimbo, pamoja na mapato ya ndani ya halmashauri.
"Leo tunaona matokeo ya uthubutu wa kuanza, leo tuna mradi wa kipekee ndani ya mkoa kuwa na jengo la gorafa linalojengwa kwa nguvu za wananchi Halmashauri na serikali kuu,nakupongeza sana Diwani na wananchi wa Uwemba" Alisema
Post A Comment: