Wafanyakazi wilayani Ludewa, mkoani  Njombe, wamepokea kwa shangwe na furaha nyongeza ya mshahara kwa watumishi wa umma, iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika maadhimisho Siku ya Wafanyakazi Duniani wilayani humo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.Dkt. Balozi Pindi Chana, amesema Rais Samia ameongeza kiwango cha chini cha mshahara kutoka Sh. 370,000 hadi Sh. 500,000.

“Taarifa kutoka kwa Mheshimiwa Rais ni kwamba mishahara imeongezwa rasmi,”amesema Dkt. Chana huku akishangiliwa na umati wa wafanyakazi waliokuwa kwenye viwanja vya maadhimisho hayo.

Aidha, Waziri Chana amekemea vikali waajiri wanaokwamisha haki za wafanyakazi na kuwataka kuwasilisha michango ya hifadhi ya jamii kwa wakati, akisisitiza kuwa agizo hilo ni la kisheria.

Ameagiza pia Wakala wa Usalama na Afya Mahala pa Kazi (OSHA) kufanya ukaguzi katika maeneo ya kazi kuhakikisha mazingira salama kwa wafanyakazi, na kubainisha kuwa Serikali iko hatua za mwisho za kuboresha mfumo wa NHIF ili kuondoa kero za sasa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Njombe, Mhe. Anthony Mtaka amewasihi wananchi kuacha maisha ya anasa na kuelekeza nguvu kwenye uwekezaji wa kilimo, biashara na misitu.\n\nKatika risala yao, Shirikisho la Vyama Vya Wafanyakazi (TUCTA) wameeleza changamoto kadhaa zikiwamo uhamisho usiozingatia haki na kutozwa fedha wakati wa kupata kadi mpya za Bima za Afya (NHIF).











Share To:

Post A Comment: