Wafanyakazi wa Sekta ya Umma na wale wa sekta binafsi nchini Tanzania wameelezwa kufurahishwa na maamuzi ya serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuongeza kima cha chini cha mishahara ya wafanyakazi wa Umma pamoja na kutangaza kuanza kwa mchakato wa mapitio ya Kima cha chini kwa wafanyakazi wa sekta binafsi nchini ili kuhakikisha mishahara yao inakuwa na viwango stahiki kulingana ma halisi halisi ya gharama za Maisha.

"Rais Samia ameweka historia kuwa Rais anayethamini utu wa mfanyakazi, ni Rais wa maendeleo ya watu, si miradi pekee. Ameonesha kuwa Serikali yame ni sikivu, yenye utashi wa kisiasa wa kweli! Mama anaendelea kusikiliza, kutatua, na kushughulikia changamoto zetu kwa dhati." Amesema  Juliana Moshi mmoja wa watumishi waliohudhuria Sherehe za Mei Mosi Singida.

Leo Alhamisi Mei Mosi, 2025 wakati wa Maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliyofanyika Kitaifa Mjini Singida kwenye viwanja vya Bombadia, Rais Samia ametangaza kuongeza Kima cha chini cha mshahara kwa asilimia 35.1 na hivyo kufanya Mtumishi aliyekuwa akipokea kiwango cha awali cha Shilingi 370,000 kupokea Shilingi 500,000 kuanzia Mwezi Julai, 2025.

"Kwa watumishi wa sekta binafsi Bodi ya Kima cha chini cha Mshahara inaendelea kufanya mapitio ili kuboresha kiwango cha chini cha mishahara." Ameongeza kusema Rais Samia.

Kufuatia maelekezo hayo ya Rais Samia, Pande zote za Nchi, watumishi mbalimbali wameshukuru kwa maamuzi hayo ya serikali, wakieleza kuwa kupanda kwa mshahara huo pamoja na ahadi ya kuendelea kupandisha madaraja watumishi mbalimbali kutaboresha Maisha yao kwa kuwafanya kuweza kumudu gharama za maisha kwa kuwa na uwezo wa kununua na kugharamia masuala mbalimbali kwa ustawi wa Maisha yao.

"Tunamshukuru sana Rais Samia na serikali yake kwa kutukumbuka. Hakika huu ni muendelezo wa hatua nyingine madhubuti za kututhamini na kutujali sisi wafanyakazi na tunamuahidi kura za kishindo kwenye uchaguzi Mkuu wa Mwezi Oktoba kama sehemu ya ahsante na shukrani zetu kwake", amesema Mwalimu Erasto Mdagasule kutoka Njombe.

Wafanyakazi hao kufuatia mabadiliko hayo ya mshahara yatakayoanza Mwezi Julai mwaka huu, wameiomba serikali kudhibiti wafanyabiashara dhidi ya kupandisha bei za bidhaa mbalimbali ili kuwafanya kufaidi kikamilifu ongezeko la mshahara huo na kuwafanya kupata nafasi ya kutekeleza shughuli na miradi mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake Mchambuzi wa masuala ya Kijamii Bwana Cyril Chaula, ameeleza kuwa hatua ya Rais Samia kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi nchini ni hatua ya kupongezwa,akieleza kuwa hatua hiyo itaongeza morali na uwajibikaji wa Wafanyakazi na hivyo kukuza ufanisi kwenye kazi utakaoleta matokeo chanya katika kufikia malengo mbalimbali yaliyowekwa na serikali.

Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

Post A Comment: