Na Denis Chambi, Tanga.
SERIKALI ya Ujerumani kupitia shirika la ufadhili wa kimataifa nchini humo 'GIZ' limetoa msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya shilingi Milion 975 vitakavyotumika katika hospitali 20 zilizopo kwenye hamashauri mbalimbali Mkoani Tanga hii ikiwa ni utekelezaji wa programu yake ya kusaidia na kuimarisha sekta ya afya hapa nchini.
GIZ ambayo inashirikiana na Wizara ya afya pamoja ofisi ya Rais tawala za mikoa na Serikali za mitaa (TAMISEMI)kwa lengo la kuboresha utoaji wa huduma bora kwa mama na mtoto pamoja na afya ya uzazi utekelezaji wake umeleta mabadiliko chanya katika vituo vya afya vilivyoguswa na mpango huo ambao umeanzishwa muda mrefu.
Akipokea vifaa hivyo Mkuu wa mkoa wa Tanga Balozi Dkt Batilda Buriani ameipongeza Serikali ya Ujerumani kupitia shirika la GIZ ambapo kupitia msaada huo unakwenda kuongeza juhudi za Serikali katika kupambana kupunguza na kuondoa kabisa vifo vya wajawazito, wakinamama pamoja na watoto wachanga waliopo chini ya miaka mitano.
"Lengo kubwa la Rais ni kupunguza vifo vya wakina mama wajawazito na watoto wachanga chini ya miaka mitano na tumeona mafanikio vifo vimepungua kwa kiasi kikubwa sana sasa wenzetu wametusaidia kupata vifaa hivi ili kuongeza vifaa tulivyonavyo na kuhakikisha kwamba watoto wetu wanaozaliwa njiti , wanaozaliwa na manjano , wanaozaliwa na changamoto ya upumuaji , wanakuwa salama tuwapongeze na kuwashukuru sana hawa wenzetu kazi hii ni kubwa na nzuri" alisema Dkt. Buriani.
Ameongeza kuwa licha ya vifaa hivyo vilivyotolewa bado kuna uhitaji kutokana na idadi kubwa ya wananchi wanaohitaji kupatiwa huduma mbalimbali ambapo ametumia nafasi hiyo kuwaomba shirika la GIZ kuangalia uwezekano wa kuendelea kuwezesha upatikanaji wa wa vifaaa vingine.
" Tumekuwa na mazungumzo na tumekubaliana kwamba waongeze vifaa hivi ni kweli tumepata vingi lakini bado uhitaji ni mkubwa tunaomba hivi vifaa vilivyopo viongezeke zaidi kutokana na idadi kubwa ya wahitaji tulionao katika vituo na hospitali zetu za halmashauri tuna imani kuwa tutaongezewa ili kuhakikisha kwamba huduma za wakina mama na watoto zinakwenda karibu zaidi na wananchi ikiwemo huduma za kibobezi" ameongeza.
Meneja wa mradi huo hapa nchini Kai Strahler-Pohl amepongeza juhudi za Serikali katika kuendelea kukabiliana na kupunguza vifo vya watoto wachanga , kuboresha matokeo ya afya wakina mama na watoto, sambamaba na kuimarisha miundombinu ya vituo vya afya.
Amesema mpango huo umelenga katika kuwezeshwa uwepo wa vifaa tiba vya kutosha kwaajili ya kuanzisha vitengo vipya vya utoaji wa huduma za utunzaji wa watoto wachanga (NCU) katika hospitali za wilaya zote zilizopo Mkoani Tanga .
" Tunafurahi sana kuimarisha huduma katika halmashauri zote za mkoa wa Tanga hasa kuweza kuzipatia hospital vitengo vya utunzaji wa watoto wachanga vinavyofanya kazi kikamilifu takribani wakazi 870,000 sasa wanaweza kuwa na uhakika kwamba Kila mtoto mchanga mvulana na msichana atatunzwa vizuri karibu na makazi yao"
" Tunathamini ushirikiano wa Serikali kupitia Wizara ya afya , TAMISEMI, mikoa halmashauri za wilaya zote pamoja na Serikali ya Ujerumani kukamilisha hili" alisema Meneja huyo.
Awali akizungumza mganga mfawidhii wa hospitali ya rufaa ya mkoa wa Tanga Bombo Dkt. Frank Shega ameishukuru shirika la GIZ kwa msaada huo ambao pia umeenda sambamaba na utoaji wa mafunzo ya utendaji wa kazi kwa baadhi ya watumishi kwa lengo la kuwaongezea maarifa na ujuzi katika utoaji wa huduma.
"Tunawashukuru na kuwapongeza sana wenzetu wa GIZ kwa kutupatia msaada wa vifaa hivi ambavyo vinakwenda kutusaidia kuhakikisha kuwa tunakuwa na vizazi hai na vyenye afya bora wamekuwa pia wakitoa mafunzo kwa watumishi kwaajili ya kuongeza weledi tumekuwa nao kwa muda mrefu na wamekuwa wadau wetu ambao wamwtusaidia sana" alisema Dkt Shega.
Post A Comment: