Timu ya mpira wa miguu ya Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA Sports Club) imeandika historia mpya baada ya kufanikiwa kupanda ligi daraja la pili(First League), kufuatia ushindi wake katika mashindano ya Ligi ya Mabingwa wa Mkoa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Sheikh Amri Abeid, Arusha.
IAA SC imethibitisha ubora wake katika mchezo wa nusu fainali kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Kajuna FC ya Kigoma. Ushindi huu muhimu umewapa tiketi ya moja kwa moja ya kushiriki Ligi Daraja la Pili (FirstLeague) msimu ujao.
Kocha wa IAA SC Abdallah Juma, ameeleza kuwa ushindi huo ni matokeo ya maandalizi ya muda mrefu na kujituma kwa wachezaji wake, na kwamba timu imepambana katika kila hatua ya mashindano na kuonyesha nidhamu kubwa ya kiuchezaji, hali iliyowasaidia kufanikisha lengo la kupanda daraja.
"Tunamshukuru Mungu kwa ushindi huu. Ilikuwa mechi ngumu lakini vijana wangu walipambana hadi mwisho. Tumefanya maandalizi kwa muda mrefu, na leo tumepata matunda yake. Kupanda daraja ni hatua kubwa kwa IAA SC, na sasa tunajipanga kwa changamoto za ligi daraja la pili" Kocha IAA SC.
Kwa upande wake nahodha wa IAA SC, Hamis Juma, amesema kuwa kupanda daraja ni heshima kwa timu na chuo kwa ujumla na ni hatua ya kwanza kuelekea malengo makubwa zaidi ya kuwa timu ya ushindani katika soka la Tanzania.
"Tumefanikisha hatua kubwa ya kupanda daraja, lakini hatutaishia hapa. Tunalenga kufanya vizuri zaidi kwenye daraja la pili na kuipeperusha vyema bendera ya IAA," Nahodha wa IAA Sports Club
Post A Comment: