Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan leo Mei Mosi, 2025 wakati wa maadhimisho ya siku ya wafanyakazi duniani, yaliyofanyika Kitaifa Mkoani Singida, ametangaza kuongeza Kima cha chini ya mishahara kwa watumishi wa Umma kutoka Shilingi 370,000 kwa Mwezi hadi shilingi 500,000 sawa na Ongezeko la asilimia 35.1%.
"Mimi na wenzangu na baada ya kuangalia uchumi ulivyopanda na ukipanda kwasababu ya nguvu zenu wafanyakazi, ninayo furaha ya kuwatangazia kwamba katika kuzidi kuleta ustawi kwa wafanyakazi, mwaka huu serikali itaongeza kima cha chini cha mshahara kwa watumishi wa umma kwa asilimia 35.1%." Amesema Rais Samia.
Akizungumzia kuhusu utekelezaji wake, Rais Samia ameeleza kuwa mabadiliko hayo mapya yataanza kutumika rasmi mwezi Julai mwaka huu, akiahidi pia mabadiliko ya mishahara kwa watumishi wa ngazi nyinginezo.
Katika hatua nyingine pia Rais Samia ameeleza kuwa bodi ya Kima cha chini cha mshahara kwa sekta binafsi inaendelea na tathmini yake ya kupitia mishahara ya sekta binafsi, akihimiza pia Wizara ya kazi pamoja na vyama vya wafanyakazi kufanya vikao na waajiri wa sekta binafsi ili kulipa mishahara kulingana na hali bora ya wafanyakazi inayohimizwa ili walau kuendana na mishahara ya kima cha chini kilichopo serikalini.
Post A Comment: