Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Innocent Bashungwa, amemwakilisha Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko, katika ufunguzi wa Mkutano wa 62 wa Bodi ya Kimataifa ya Uhamasishaji wa Uwazi na Uwajibikaji katika Usimamizi wa Rasilimali za Madini, Mafuta na Gesi Asilia (EITI), uliofanyika katika Hoteli ya Gran Melia jijini Arusha, leo tarehe 13 Machi 2025.

Mkutano huo umehudhuriwa na viongozi mbalimbali, wakiwemo Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, pamoja na Wajumbe wa Bodi ya EITI kutoka mataifa mbalimbali duniani, wakiwemo wawakilishi wa kampuni kubwa zinazojihusisha na uchimbaji na utafutaji wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia, pamoja na asasi za kiraia.

Akifungua mkutano huo, Waziri Bashungwa alisema kuwa kufanyika kwa mkutano huo nchini ni fursa adhimu ya kuonesha jinsi Tanzania inavyotekeleza vigezo vya kimataifa vya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa rasilimali za madini, mafuta na gesi asilia kupitia sheria inayosimamia uwazi na uwajibikaji.

"Nimshukuru Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuhakikisha Tanzania ni moja ya nchi wanachama wa EITI zinazotekeleza masuala ya uwazi wa mapato yanayolipwa na kampuni zinazofanya shughuli katika sekta ya madini, mafuta na gesi asilia," amesema Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ametumia fursa hiyo kuwahakikishia Watanzania, wawekezaji, na wageni kutoka nje ya nchi kuwa Tanzania ni nchi yenye amani, utulivu zikiwemo fursa nyingi, na ni mahali sahihi kwa uwekezaji katika sekta mbalimbali, ikiwemo sekta ya utalii.

Pia, Bashungwa amempongeza Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, kwa kuendelea kusimamia kikamilifu utekelezaji wa maono ya Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuleta mageuzi makubwa na kuweka uwazi katika usimamizi wa rasilimali za nchi.

Naye, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde, amesema kuwa kufanyika kwa mkutano huo wa kimataifa ni kielelezo cha kazi nzuri zinazofanyika chini ya uongozi wa Mhe. Rais Dkt. Samia, ambazo zimevutia mikutano mingi ya aina hii kufanyika nchini.

Mavunde ameongeza kuwa Tanzania ni mdau mkubwa wa uwazi na uwajibikaji katika Sekta ya Uziduaji, jambo ambalo limechangia kuifanya nchi kuwa mwenyeji wa mkutano huo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi wa Shughuli za TEITI, CPA Ludovick Utouh, ameeleza kuwa mkutano huo wa Bodi ya Wakurugenzi wa Uwazi na Uwajibikaji katika Sekta ya Uziduaji Kimataifa (EITI) unahusisha wanachama 57 kutoka mataifa mbalimbali duniani.




Share To:

Post A Comment: