Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza imeandaa Mkakati madhubuti wa kuandaa Filamu tano ambazo zitaelezea utamaduni, vivutio vya ndani, historia na kuhamasisha uzalendo na utaifa kwa vizazi vijavyo.
Hayo yameelezwa na Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro Oktoba 23, 2024 Bungeni Jijini Dodoma wakati akiwasilisha taarifa kuhusu Mikakati madhubuti ya kukuza Sanaa nchini hususani tasnia ya Filamu, kwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo chini ya Mwenyekiti Mhe. Husna Sekiboko.
Mhe. Ndumbaro amezitaja Filamu hizo kuwa ni Filamu ya Chifu Kingalu, Filamu ya Asante, Filamu ya Mwalimu Nyerere na Tamthilia inayohusu masuala ya Bima na Filamu ya A Trip With Your Wife, lengo likiwa ni kuitangaza Tanzania katika nyanja mbalimbali kupitia Filamu na kuwatafutia soko wadau wa filamu nje ya Tanzania.
"Kwa sasa Bodi inakamilisha Mkakati wa kuunganisha Mfumo wa kidigiti wa (Arts Management Information System - AMIS) na mifumo mengine ya TAUSI kutoka TAMISEMI, COSOTA NIDA, BRELA na TRA ili kiwafikia wadau bila kuwa na haja ya kufika ofisi za Bodi kupata huduma" amesema Mhe. Ndumbaro.
Wakichangia taarifa hiyo, Wajumbe wa Kamati wameelekeza wizara kupitia Bodi ya Filamu, kutengeneza mpango mahususi wa kuunga mkono uandaaji na usambazaji wa Filamu za Tanzania pamoja na kuwafikia wasanii walioko vijijini.
Post A Comment: