Halmashauri ya Mji Njombe imepongezwa kwa usimamizi mzuri wa sheria, kanuni na miongozo ya Serikali ambayo imeiwezesha Halmashauri ya Mji Njombe kupata hati safi kwa Hesabu za mwaka 2022/2023 kutoka kwa Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).


Pongezi hizo zimetolewa na Katibu Tawala Mkoa wa Njombe Bi.Judica Omari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Njombe Mhe.Anthony Mtaka, katika Mkutano Maalum wa Baraza la Madiwani uliokaa kwa ajili ya kujadili Majibu na Utekelezaji wa Hoja za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

“Ninawapongeza sana Baraza la madiwani, Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Menejimenti na wataalamu wote wa Halmashauri kwa usimamizi wa sheria, kanuni na miongozo ya Serikali, usimamizi mziri wa ukusanyaji wa mapato na usimamizi wa miradi ya maendeleo ambao umewezesha Halmasahuri ya Mji Njombe kupata hati safi kwenye hesabu kuu za Halmashauri, Mfuko wa afya wa pamoja na mfuko wa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu”. Alisema Bi Judica Omari ,Katibu Tawala Mkoa wa Njombe.

Aidha ameielekeza Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Njombe, kushirikiana na Baraza a madiwani kuyafanyia kazi mapungufu yanayosababisha kutokea kwa hoja haswa kwenye ukusanyaji wa mapato, ufuatiliaji wa madeni ya mikopo ya asilimia 10 inayotolewa kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu pamoja na kuhakikisha madeni ya wazabuni na watumishi yanalipwa kwa wakati.

Halmashauri ya Mji Njombe kwa miaka 5 mfululizo kuanzia mwaka wa fedha 2018/2029 – 2022/2023 imeendelea kupata hati safi kwenye Hesabu kuu za Halmashauri, Hesabu za mradi wa mfuko wa Afya wa pamoja (Health Sector Busket Fund) na Hesabu za Mfuko wa Wanawake,Vijana na Watu wenye Ulemavu (WYDF).
Share To:

Post A Comment: