MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Mpango ameielekeza Wizara ya Madini na Taasisi zake kuelekeza nguvu katika mikoa yenye madini mkakati ikiwemo Dodoma kufanyiwa utafiti wa kina wa haraka ili kufikia asilimia 50 kabla ya mwaka 2030.

Dkt. Mpango ameyasema hayo leo Juni 20, 2024 katika ufunguzi wa Kongamano la Wachimbaji Madini wakati akitembelea mabanda ya maonesho yanayokwenda sambamba na mkutano wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA) lililoanza leo hadi Juni 27 katika viwanja vya Jakaya Kikwete Conventional Centre (JKCC) mkoani Dodoma.

Amesema kwamba mkakati wa Wizara kupitia vision 2030: yenye kauli mbiu ya MADINI NI MAISHA NA UTAJIRI ni lazima ijielekeze katika kipaumbele cha  kubaini madini mkakati yaliyopo ili nchi iwezi kunufaika na madini hayo ambayo kwasasa yana uhitaji mkubwa Duniani kutokana na mrengo wa Nishati Safi na kupunguza uchafuzi wa mazingira kupitia hewa ya ukaa.

Akizungumzia mazingira ya uwekezaji Dkt. Mpango amesema, Serikali imeendelea kuboresha mazingira ya biashara ya Madini kwa wachimbaji wadogo ambapo sasa idadi ya vituo vya ununuzi wa madini imefikia 100 na masoko ya madini 42.

Ameongeza kuwa, uchimbaji mdogo wa madini unagusa moja kwa moja maisha ya watu huku miongoni mwa mazingira bora ya uwekezaji ni uchumi imara, hali ya utulivu, uwepo wa amani na sheria rafiki.

Akimkaribisha Mgeni Rasmi,Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema Wizara ya Madini imeweka kipaumbele kwenye utafiti wa Kina na hasa wa Madini mkakati na kwamba utekelezaji wake utafanyika kupitia miradi mikubwa iliyopangwa kutekelezwa na kwa sasa wizara imejipanga kununua helicopter kwa ajili ya utafiti wa kina wa madini.

Naye Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania(FEMATA) Ndg. John Wambura Bina ameishukuru serikali kwa kuwa karibu na wachimbaji wadogo na ushirikiano mkubwa inaoutoa na kuwasilisha ombi la serikali kuweka mazingira rafiki kuruhusu uingizwaji wa madini kutoka nje ya nchi sambamba na uanzishwaji wa Soko la Madini Zanzibar ili kulifikia soko la watalii.

Share To:

Post A Comment: