Tanzania imetangaza azma yake ya kuwania nafasi ya uanachama usio wa kudumu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030, huku ikiahidi kupeleka katika chombo hicho sauti imara ya Afrika na kusukuma mbele diplomasia ya kuzuia migogoro, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani na mageuzi ya operesheni za kulinda amani.
Msimamo huo umetolewa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika Mjadala wa Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, unaofanyika jijini New York, Marekani.
Mhe. Ndejembi amesema Tanzania ikichaguliwa itatoa kipaumbele kwa diplomasia ya kuzuia migogoro kabla haijawa vita, utatuzi wa migogoro kwa njia za amani, kuimarisha nafasi ya wanawake katika ulinzi na ujenzi wa amani, kuongeza ushiriki wa vijana katika ajenda za amani na usalama, pamoja na kusukuma mbele mageuzi ya operesheni za Umoja wa Mataifa za kulinda amani.
Tanzania imesema dhamira hiyo imepata uungwaji mkono wa Umoja wa Afrika (AU), huku uchaguzi ukitarajiwa kufanyika Juni 2028.
Katika hotuba ya Makamu wa Rais, Tanzania imeweka wazi msimamo kwamba Umoja wa Mataifa unapaswa kuendelea kufanyiwa mageuzi ili kuimarisha misingi ya haki, usawa na uwakilishi wenye uwiano, badala ya mfumo wa kimataifa kuendelea kuakisi zaidi nguvu na ushawishi wa mataifa machache.
Tanzania imesisitiza kuwa mageuzi hayo ni muhimu katika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na migogoro na vita, athari za mabadiliko ya tabianchi, milipuko ya magonjwa, kasi ya maendeleo ya Akili Mnemba (AI), pamoja na changamoto za usalama wa nishati.
Makamu wa Rais amesema, Tanzania imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuongeza kiwango cha uzazi unaofanyika katika vituo vya afya kutoka asilimia 51 mwaka 2015 hadi asilimia 81 mwaka 2022. Amesema uzoefu katika hilo unaonyesha kuwa uwekezaji katika miradi inayotekelezeka na kuweka ustawi wa watu mbele, maendeleo yanaweza kuhama kutoka hatua ya ahadi hadi matokeo yanayoonekana na kupimika.
Amesema ni kwa msingi huo ambapo Rais Samia Suluhu Hassan alikubali jukumu la kuwa kinara wa masuala ya Afya ya Mama na Mtoto kwa niaba ya Umoja wa Afrika. Chini ya uongozi wake, Tanzania imefanikiwa kupunguza vifo vya akina mama kwa asilimia 80 ndani ya kipindi cha miaka saba pekee. Tanzania inalenga kufikia malengo ya "Sifuri Tatu" (Three Zeros), ambayo ni: Kutokuwepo kwa vifo vya mama na mtoto vinavyoweza kuzuilika; kutokuwepo kwa uzazi unaofanyika majumbani; na kutokuwepo kwa watoto ambao hawajapata chanjo. Amesema uzoefu unaonyesha kuwa hilo ni lengo ambalo Afrika inaweza kulifikia kwa mafanikio, lakini litahitaji uongozi thabiti wa kisiasa, rasilimali fedha za kutosha, na ushirikiano imara zaidi. Hivyo, amehimiza Jumuiya ya Kimataifa kuungana nasi katika kulisukuma mbele ajenda hiyo.
Tanzania pia imesisitiza umuhimu wa nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa zaidi katika taasisi na mifumo ya kimataifa inayofanya maamuzi ya kifedha yanayoathiri uchumi wake wa muda mrefu wa maendeleo, Tanzania imewasilisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 kama msingi wa kujenga uchumi jumuishi, shindani na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko, kupitia uwekezaji katika watu, miundombinu yenye tija, teknolojia, ubunifu, wanawake na vijana.
Makamu wa Rais amesema ni muhimu kufanyika kwa mageuzi kwenye mfumo wa fedha wa kimataifa ili nchi zinazoendelea ziweze kupata rasilimali zinazohitajika kuharakisha utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs). Amesema Tanzania inasisitiza kuongezeka kwa mikopo yenye masharti nafuu, kuhamasishwa kwa uwekezaji wa sekta binafsi, kurahisishwa kwa upatikanaji wa fedha za maendeleo na tabianchi na nchi zinazoendelea kupewa sauti kubwa katika maamuzi ya kifedha duniani.
Katika ajenda ya mabadiliko ya tabianchi, Tanzania imeeleza wasiwasi kuhusu pengo kati ya kiwango cha uzalishaji wa gesi chafuzi duniani na fedha zinazotolewa kusaidia nchi zinazoathirika kukabiliana na madhara yake.
Tanzania imesisitiza kuwa nchi zinazochangia kwa kiwango kikubwa uzalishaji wa gesi chafuzi zinapaswa kubeba wajibu mkubwa zaidi katika kugharamia hatua za kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Katika kueleza mkakati wake wa mpito kuelekea nishati safi, Tanzania imetaja Bwawa la Kufua Umeme la Julius Nyerere lenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115, miradi ya nishati ya jua na upepo yenye jumla ya megawati 650, pamoja na mipango ya kuzalisha megawati 130 za nishati ya jotoardhi.
Pia imetaja uwekezaji katika reli ya umeme na lengo la kufikisha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika asilimia 80 ya kaya ifikapo mwaka 2034.
Katika eneo la diplomasia ya kimataifa, Makamu wa Rais amesema Tanzania inapinga matumizi ya vikwazo vya upande mmoja vinavyowekwa na baadhi ya mataifa dhidi ya mengine, ikisema hatua hizo zinaweza kudhoofisha mamlaka ya nchi, kuathiri maendeleo na kupunguza uwezo wa wananchi kunufaika kikamilifu na haki zao
Tanzania imeeleza mshikamano wake na Cuba, Zimbabwe na mataifa mengine yanayokabiliwa na vikwazo hivyo, huku ikitoa wito wa kuchukuliwa hatua za makusudi kuelekea kuondolewa kwa vikwazo bila masharti.
Kuhusu hali ya Gaza na Mashariki ya Kati, Tanzania inasisitiza umuhimu wa kuwalinda raia, kuruhusu misaada ya kibinadamu kuwafikia wanaohitaji bila vikwazo na kurejesha diplomasia kuwa njia kuu ya kutafuta amani ya kudumu.
Kwa ujumla, ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa 81 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa umeunganisha ajenda ya kitaifa ya maendeleo na hoja pana kuhusu nafasi ya Afrika katika mfumo wa kimataifa.
Tanzania imesisitiza kuwa Umoja wa Mataifa haupaswi kuwa jukwaa linaloakisi pekee uwiano wa nguvu duniani, bali taasisi inayosimamia haki, mshikamano, usawa na maendeleo kwa mataifa yote.
Ni msimamo unaoweka bayana ajenda ambayo Tanzania inakusudia kuibeba katika safari yake ya kuwania nafasi katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwa kipindi cha 2029–2030: kuimarisha sauti ya Afrika, kuzuia migogoro, kutetea suluhu za amani na kusukuma mageuzi ya mfumo wa kimataifa ili uwe na uwakilishi wenye uwiano zaidi.
Imetolewa na
Ofisi ya Makamu wa Rais
New York – Marekani
23 Septemba 2026.
>AWATAKA WATUMISHI KUACHA KUFANYA KAZI KWA MAZOEA
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka watumishi wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira kuongeza bidii, uwajibikaji na kuachana na utendaji wa kazi kwa mazoea ili kuhakikisha majukumu ya Serikali yanatekelezwa kwa ufanisi na kwa wakati.
Makamu wa Rais ametoa wito huo leo, alipofanya ziara yake ya kwanza katika Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), iliyopo Mtumba, jijini Dodoma, ambako alipokelewa na wafanyakazi pamoja na Menejimenti ya Wizara hiyo.
Amesisitiza umuhimu wa watumishi kubadili mitazamo na namna ya kufanya kazi, akitaka kila mmoja kuwa mbunifu na kuweka mipango inayolenga kuleta matokeo yanayoonekana kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.
Makamu wa Rais amewasihi watumishi kutumia nafasi zao kutoa huduma yenye thamani kwa watanzania na kutambua dhamana waliyonayo katika kuwahudumia wananchi. Pia amewataka kubadili mitazamo na namna ya kufikiri, kuwa wabunifu na kuhakikisha mipango inayowekwa inaleta tija na matokeo chanya katika shughuli mbalimbali zinazotekelezwa kwa maslahi mapana ya Taifa.
Halikadhalika, amewataka kuongeza jitihada katika kudumisha Muungano kwa kuwa na mipango endelevu inayolenga kutatua changamoto mbalimbali pamoja na kutoa elimu ya fursa zilizopo katika Muungano.
Amewasihi Viongozi na Watumishi wa Wizara hiyo, kuwa na mipango endelevu katika utekelezaji wa ajenda ya ulinzi na uhifadhi wa mazingira kwa kutumia vema kampeni za upandaji miti, usafi wa majiji na miji kwa kuweka nyenzo zitakazosaidia kufanya hali hiyo kuwa endelevu. Vile vile amesisitiza umuhimu wa kuwa na Mpango maalum utakao saidia wananchi kuhama katika shughuli za kila siku zinazoharibu mazingira.
Awali, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhandisi Hamad Masauni, amempongeza Makamu wa Rais kwa kuaminiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika nafasi hiyo na kumhakikishia ushirikiano katika kutekeleza majukumu mbalimbali yanayohusu Ofisi ya Makamu wa Rais.
Akiwasilisha taarifa kuhusu shughuli zinazotekelezwa na idara mbalimbali zilizo chini ya Ofisi ya Makamu wa Rais, Katibu Mkuu, Ofisi ya Makamu wa Rais Dkt. Richard Muyungi, amesema wizara hiyo ina Idara nne, Vitengo nane na Taasisi mbili zinazotekeleza majukumu mbalimbali, ikiwemo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 katika masuala ya Muungano na Mazingira.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi akiwa katika picha ya pamoja na Mkurugenzi Mkuu waBaraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. EmmaculateSware pamoja na Watumishi waliofanya kazi pamoja na Makamu wa Raiswakati akifanya kazi Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira(NEMC). Picha hiyo imepigwa mara baada ya Makamu wa Rais kukamilishaziara aliyoifanya Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Mikocheni Jijini Dar es Salaam, leo tarehe 02 Julai 2026. 

Serikali imezitaka Wizara, Taasisi za Umma, Sekta Binafsi, Watafiti na Mashirika ya Kiraia kuchangamkia fursa ya Tanzania kuwa mwenyeji wa 12 wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Nairobi (COP 12).
Hayo yamesemwa leo Julai 2, 2026 Jijini Tanga na Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Reuben Kwagilwa wakati akitoa tamko la Serikali kuhusu maandalizi ya Tanzania kuelekea Mkutano huo unaotarajia kufanyika nchini kuanzia tarehe 6-9 Oktoba mwaka huu.
Naibu Waziri Kwagilwa amesema katika Mkutano wa 11 wa Nchi Wanachama uliofanyika nchini Madagasca mwaka 2024, Tanzania ilichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Kamati Tendaji ya Mkataba wa Nairobi kwa kipindi cha miaka miwili hadi Disemba Mwaka 2026 pamoja na kuteuliwa kuwa mwenyeji wa COP12.
“Mkutano wa COP12 utajadili utekelezaji wa Mpango Kazi wa Mkataba kwa kipindi cha mwaka 2024–2026 pamoja na kujadili masuala muhimu ikiwemo hifadhi na urejeshwaji wa mifumo ikolojia ya bahari kama mikoko, miamba ya matumbawe na nyasi bahari” amesema Mhe. Kwagilwa.
Ameongeza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuipa kipaumbele sekta ya mazingira na uhifadhi wa rasilimali za bahari ili kuimarisha uhifadhi wa rasilimali za bahari, mito, maziwa, maji chini ya ardhi na maeneo oevu.
Kwa mujibu wa Naibu Waziri Kwagilwa, amesema Dira 2050 imeitambua sekta ya uchumi wa Buluu kuwa miongoni mwa sekta za kimkakati zinazokusudia kuleta mageuzi ya maendeleo endelevu na kuchangia ukuaji wa kijamii, kiuchumi na kiikolojia.
Amesema kuwa Tanzania ni nchi ya pwani yenye fursa kubwa ya kunufaika na sekta ya uchumi wa buluu kupitia uvuvi, nishati, usafirishaji, utalii, madini, mazingira na viwanda, hivyo mkutano huo utaliwezesha taifa kuwa katika nafasi bora ya kufikia maendeleo endelevu.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Burian amesema matokeo ya utafiti uliofanyika mkoani humo yanaonyesha athari za mabadiliko ya tabianchi zimeanza kuathiri kwa kiwango kikubwa shughuli za uvuvi na ukuzaji wa viumbe maji, hususan kilimo cha mwani.
Amesema utafiti uliofanyika kati ya mwaka 2021 na 2025 umebaini kuwa joto la bahari limeongezeka kutoka nyuzi joto 25.6 mwaka 2021 hadi kufikia nyuzi joto 28.39 mwaka 2024, hali inayobadili mfumo wa ikolojia wa bahari na kuathiri uzalishaji katika sekta ya uvuvi.
"Tumeshuhudia ongezeko la karibu nyuzi joto tatu baharini, huku siku za wavuvi kwenda kuvua zikishuka kutoka siku 221 mwaka 2021 hadi siku 170 kutokana na upepo mkali na hatari ya usalama baharini. Pia mavuno ya samaki yamepungua kwa wastani wa asilimia 25 hadi 30," amesema Dkt. Burian.
Awali akimkaribisha mgeni rasmi, Naibu Katibu Mkuu (Mazingira) Ofisi ya Makamu wa Rais, Balozi Baraka Luvanda amesema mkutano wa COP 12 utahusisha washiriki takribani 500-600 ikiwemo viongozi wa nchi, wataalamu na wadau mbalimbali.
Ameongeza kuwa lengo la tamko hilo la Serikali ni kuweka msingi wa maandalizi ya kina, ikiwa ni pamoja na kubainisha vipaumbele vya Taifa, na kupanga mikakati ya ushiriki ili kuhakikisha maandalizi yanafanyika kwa ufanisi na kwa wakati.
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni nchi mwanachama wa Mkataba wa Nairobi unaohusu Hifadhi, Usimamizi na Uendelezaji wa Mazingira ya Bahari na Ukanda wa Pwani wa Magharibi mwa Bahari ya Hindi.
Mkataba huu ulisainiwa tarehe 21 Juni 1985 na unatekelezwa chini ya usimamizi wa Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP).
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni amesema vijana wanapaswa kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kwa kukuza ubunifu, kuongeza bidii katika kazi, kutumia teknolojia na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi hususan zilizo rafiki kwa Mazingira.
Mhe. Masauni amesema hayo katika Kongamano la Vijana lililofanyika jijini Dar es Salaam, Juni 2, 2026 ambalo ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani ambapo kilele chake kitaifa yanafanyika Juni 5, 2026 mkoani Dodoma.
Amesema, kongamano hilo ni jukwaa muhimu linalowaunganisha vijana na maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani kwa kuwapa nafasi ya kushiriki katika mijadala, kujifunza kutoka kwa wataalam, kubadilishana uzoefu na kuibua suluhisho bunifu zinazoweza kutekelezwa kwa vitendo katika jamii zao.
“Ninyi ndio nguvu kazi ya Taifa na nguzo muhimu katika mapambano dhidi ya uharibifu wa mazingira. Kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, vijana ni zaidi ya asilimia 64 ya nguvu kazi ya Taifa. Hii ina maana kuwa mchango wenu ni muhimu sana katika kulinda mazingira, kukuza uchumi wa kijani na kuhakikisha maendeleo endelevu ya Taifa letu.”
Aidha ameongeza kuwa ni vyema vijana wakatambua changamoto za kimazingira pia zinaweza kuwa fursa kubwa za kiuchumi, takwimu za kimataifa zinaonesha kuwa mpito kuelekea uchumi wa kijani unaweza kuzalisha ajira milioni 8.4 kwa vijana duniani ifikapo mwaka 2030.
Aidha, amesema uchumi endelevu duniani unakadiriwa kuwa na thamani ya zaidi ya dola trilioni 12 na uwezo wa kuzalisha zaidi ya ajira milioni 380 duniani kote.
“Hii inaonesha dhamira ya pamoja ya Taifa katika kulinda mazingira na kuhakikisha matumizi endelevu ya rasilimali za asili kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho”.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais, Dkt. Richard Muyungi, amesema kuwajengea uwezo vijana kupitia programu za kujitolea ni mkakati muhimu wa kuandaa kizazi kitakachosimamia agenda za maendeleo endelevu, uhifadhi wa mazingira na uchumi wa kijani.
Amesema programu za kujitolea zinawawezesha vijana kupata uzoefu wa kazi unaohitajika katika soko la ajira, huku zikizisaidia taasisi kupata kundi la vijana wenye maarifa, ubunifu na uwezo wa kutumia teknolojia katika kutatua changamoto mbalimbali za maendeleo.
“Afrika ina hazina kubwa ya rasilimali watu, ambapo takribani asilimia 40 ya vijana wa dunia wanaishi katika bara hilo, jambo linalotoa fursa kubwa ya kuharakisha maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiteknolojia endapo vijana hao watapatiwa elimu, ujuzi na nafasi za kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.” Amesema Dkt. Muyungi.
Ofisi ya Makamu wa Rais inatarajiwa kuzindua Programu ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kimkakati ya Mazingira Endelevu Tanzania katika kilele cha Siku ya Mazingira Duniani (WED) ambapo kitaifa itafanyika jijini Dodoma, Juni 5, 2026.
Akizungumza katika uzinduzi wa usafi wa Mazingira kuelekea siku hiyo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais Mhe. Mhandisi Hamad Yussuf Masauni alisema lengo ni kuhakikisha Tanzania inakuwa nchi ya mfano duniani katika suala la Uhifadhi na Utunzaji wa Mazingira.
Alisema Programu hiyo inalenga kutekeleza Dira, 2050 hususan nguzo ya tatu kuhusu Uhifadhi wa Mazingira na Ustahimilivu wa Mabadiliko ya Tabianchi ikiwa na lengo la kupanda miti bilioni 2 kwa mwaka, kuimarisha Biashara ya Kaboni, Uanzishaji wa Bustani za Kijani katika Miji na shughuli zingine za Kijani.
“Pia program hii inatarajia kuongeza ajira zinazoweza kufikia zaidi ya elfu ishirini na tano (25,000) ifikapo 2030 kupitia sekta za taka, misitu, kaboni na nishati safi,”alisema Mhe. Masauni.
Alifafanua kuwa tukio hilo ni sehemu ya juhudi za Kitaifa na Kimataifa za kulinda mazingira, kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi na kujenga jamii yenye afya na ustahimilivu.
Aidha, alileza Dira, 2050 imeweka maono ya Taifa kuwa hadi kufikia mwaka 2050 Tanzania iwe kinara katika matumizi endelevu ya rasilimali, Taifa linalotumia taka kama malighafi kwa manufaa ya kiuchumi na Taifa kinara katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kwa kuimarisha ustahimilivu na uendelevu wa mazingira.
“Juhudi zinahitajika ili kutekeleza shughuli za mazingira kwa njia jumuishi inayohusisha makundi yote ya kijamii bila kujali jinsia au umri. Kwa jiji la Arusha, tafiti za mwaka 2020 zinaonesha kuwa jiji linazalisha takribani tani 550 za taka ngumu kwa siku, ambapo zaidi ya asilimia 60 ya taka hizo zinaweza kurejelezwa ikiwa zitadhibitiwa vizuri kupitia uchumi rejeshi,"aliongeza.
"Kwa ngazi ya Kitaifa, Tanzania inakadiriwa kupoteza takribani hekta 469,420 za misitu kila mwaka kutokana na shughuli mbalimbali zisizo endelevu ikiwa ni pamoja na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, kilimo kisicho endelevu, ufugaji holela pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu zinazosababisha uharibifu wa mazingira hali inayochangia kuongezeka kwa gesi joto, kuharibu vyanzo vya maji na kuhatarisha usalama wa bioanuwai,".
Alieleza Upandaji wa miti yenye matumizi mbalimbali una mchango mkubwa katika kufyonza gesi ya kaboni, kupunguza mmomonyoko wa udongo, kuhifadhi vyanzo vya maji, kutoa matunda pamoja na kuongeza kipato kwa wananchi kupitia bishara ya Kaboni na kuongeza ustahimilivu dhidi ya athari za Mabadiliko ya Tabianchi.
"Matumizi ya nishati safi ya kupikia ni hatua muhimu katika kupunguza utegemezi wa kuni na mkaa ambao umeendelea kuwa miongoni mwa sababu kuu za uharibifu wa misitu nchini.
“Kuimarisha upatikanaji na matumizi ya nishati safi kama vile gesi asilia, umeme, biogas na teknolojia bora za kupikia kutasaidia kupunguza kasi ya ukataji miti, kupunguza uzalishaji wa gesi joto na kuboresha afya za wananchi hususan wanawake na watoto ambao huathirika zaidi na moshi unaotokana na matumizi ya nishati isiyosafi," alisisitiza.
Naye Mkuu wa Wilaya Arusha Mhe. Joseph Mkude alisema kila mmoja ana wajibu wa kutunza na kuhifadhi mazingira na kuzingatia matumizi ya nishati safi ya kupikia na kusema taasisi nyingi zinatekeleza agizo hilo.
Amesema arusha imekuwa ikifanya kila jitihada kuhakikisha jiji hilo linakuwa safi na kushirikisha jamii yote kutambua umuhimu wa utunzaji wa mazingira ndio maana wanafunzi wamepewa kipaumbele.









































