Na Hamida Kamchalla, TANGA.
WAKULIMA wameshauriwa kutumia Kilimo Ekolojia ili kujiweka wao na walaji wa mazao yao katika hali ya usalama ikiwa ni pamoja na kujitengenezea masoko ya Kimataifa.
Ofisa Mtetezi wa Kampuni ya Tanzania Organic Agriculture Movement (TOAM), Paul Chilewa ametoa ushauri huo katika Maadhimisho ya Kitaifa ya wiki ya Siku ya Chakula Duniani katika viwanja vya shule ya sekondari Usagara jijini Tanga.
Chilewa amesema TOAM ina wadau mbalimbali ambao wanajishuhulisha na utengenezaji wa bidhaa za kilimo hai kama vile mbolea hai, viuatilifu hai lakini pia mbegu hai.
Kwa mujibu wa Chilewa TOAM na wadau hao kwa kushirikiana na wadau wa kilimo wanatekeleza mkakati wa kilimo Ekolojia hai wa mwaka 2023 hadi 2030 ambao una vipaumbele kadhaa.
"Kipaumbele cha kwanza ni kuhakikisha pembejeo hai zinawafikia wakulima, hapa tuna TBPL hawa wana mbolea na viuatilifu hai ambavyo, kwa Mkoa wa Tanga na mingine vinafaa kwa sababu haviachi mabaki kwenye mazao,
"Kuna changamoto kubwa ukipita dawa kwenye mazao viuatilifu vinabakiza kemikali ambazo nyingi zina madhara kwa afya ya maji, hivyo tunawasisituza wakulima watumie ambayo ni hai haiachi mabaki wala haiathiri udongo" amesema.
Sambamba na hilo amesema suala la masoko limezingatiwa kwa kiwango kikubwa kwani kuanzia masoko ya ndani hadi ya nje ya nchi yanaangalia sana mazao ambayo hayatumii pembejeo zenye kemikali.
Amebainisha kwamba, "ili kuifikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050, tunalazimika kuwa na watu wenye nguvu na afya iliyo bora, ukiachia mbali masoko hata sisi wenyewe inatupasa kuzitumia na kula vyakula salama" amesisitiza Chilewa.
Kwa upande wake Mgunduzi wa mbolea ya miamba, Donald Mwakamele, ameeleza kuwa mbolea hiyo imetengenezwa kwa kutumia miamba pekee bila kuchanganywa na kemikali yoyote, lengo likiwa kurejesha udongo katika uasilia wake na kuupatia virutubisho vyote muhimu pamoja na vitamini vinavyohitajika na mimea.
Mgunduzi wa mbolea ya Miamba kutoka kutoka Mkoani Songwe Donald Mwakamele akielezea kuhusu mbolea hiyo kwenye maadhimisho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea kufanyika kitaifa mkoani Tanga.Mwakamele amebainisha kuwa tofauti na mbolea za kawaida zinazomlazimisha mkulima kununua kila msimu, mbolea hii ya miamba ina uwezo wa kudumu udongoni kwa muda wa miaka mitatu, hatua inayopunguza kwa kiasi kikubwa gharama za uzalishaji kwani mkulima ana uwezo wa kulima na kuvuna kwa kipindi chote hicho bila kuweka mbolea tena.
"Kiwanda cha mbolea hiyo kilichopo mkoani Songwe tayari kimefunguliwa na kuanza uzalishaji, huku matokeo chanya yakianza kuonekana katika maeneo mbalimbali kama vile Moshi, Njombe, na Songea ambako mbolea hiyo imefanya vizuri katika kuboresha mazao na kurudisha madini halisi ya ardhi", amesema.
Wananchi mbalimbali wakiendelea kupata elimu katika maadhimisho ya siku ya chakula Duniani yanayoendelea kufanyika kitaifa mkoani Tanga katika viwanya vya Shule ya Sekondari Usagara.



Post A Comment: