Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) imesisitiza umuhimu wa kuhakikisha elimu ya uwekezaji inawafikia wananchi wote bila kujali hali zao za kimwili au uwezo wa kiuchumi, ili kuongeza ushiriki wa wananchi katika masoko ya mitaji nchini.


Akizungumza jijini Dar es Salaam leo wakati wa mafunzo ya elimu ya fedha kwa watu wenye ulemavu, Mkuu wa Uhusiano wa Umma wa CMSA, Charles Shirima, amesema kuwa kuwawezesha wananchi kupata maarifa ya kifedha ni hatua muhimu katika kuongeza akiba za ndani na kukuza uchumi jumuishi.

"kampeni hii ni sehemu ya maadhimisho ya Wiki ya Wawekezaji Duniani (World Investor Week), mpango wa kimataifa unaoratibiwa na Shirika la Kimataifa la Tume za Dhamana (IOSCO) kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu uwekezaji salama na wenye taarifa sahihi",amesema Shirima


Amesema kuhamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki katika uwekezaji ni muhimu katika kujenga utajiri binafsi na kuimarisha uchumi wa taifa.


Shirima amesema kuwa CMSA imeshirikiana na Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA) kutoa mafunzo yatakayowawezesha washiriki kuelewa fursa mbalimbali za uwekezaji na namna ya kuzitumia kuboresha maisha yao.



"Mafunzo hayo yamejikita katika namna masoko ya mitaji yanavyofanya kazi, utaratibu wa kununua hisa pamoja na mbinu bora za kusimamia fedha binafsi",amesema Shirima


Aidha, Shirima amesema CMSA hutumia njia mbalimbali kufikisha elimu hiyo kwa wananchi, zikiwemo warsha za ana kwa ana, semina za mtandaoni na mitandao ya kijamii, huku makundi yanayolengwa yakijumuisha wanafunzi, walimu, viongozi wa maeneo na wananchi kwa ujumla.


Amesema lengo ni kujenga mazingira jumuishi ya uwekezaji kwa kuhakikisha wananchi wa makundi mbalimbali wanapata maarifa na fursa za kushiriki katika masoko ya mitaji.

Kwa upande wake, Katibu Mkuu wa SHIVYAWATA, Jonas Mbago, amesema mafunzo hayo yamesaidia kurahisisha dhana za kifedha ambazo awali zilionekana kuwa ngumu kueleweka, huku yakiwafahamisha washiriki njia mbadala za kusimamia na kukuza akiba zao.


Mbago amesema watu wengi katika jamii wamekuwa na mazoea ya kuhifadhi fedha majumbani au kwenye akaunti za benki zenye riba ndogo, hali inayoweza kupunguza fursa za kukuza fedha zao.



“Mafunzo haya yametutambulisha katika njia mpya za uwekezaji zinazoweza kuboresha usalama wetu wa kifedha,” amesema, huku akiiomba Serikali kupanua programu kama hizo ili kuwafikia wananchi wengi zaidi nchini.


Naye Mwenyekiti wa chama kinachowakilisha watu wenye 'Psoriasis', ugonjwa sugu wa ngozi unaosababisha kutokea kwa mabaka mazito yenye magamba, Dorothy Malechela, amesema wananchi wanapaswa kuachana na tabia ya kuhifadhi fedha bila kuzizalisha na badala yake kujifunza fursa za uwekezaji zinazodhibitiwa kisheria.


Amesema mipango sahihi ya kifedha inaweza kuwasaidia watu kukuza biashara zao, kuimarisha usalama wa kifedha na kufikia malengo yao ya muda mrefu.











Share To:
Next
This is the most recent post.
Previous
Older Post

OSCAR ASSENGA

Post A Comment: