Waziri wa Madini Anthony Mavunde amesema  kuwa serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluh Hassan imejipanga katika mwaka wa fedha 2024/25 kuanza ujenzi wa maabara kubwa na ya kisasa na yenye vifaa vya kisasa itakayojengwa katika eneo la Kizota jijini Dodoma ili kuendana na kasi ya ukuaji wa Sekta ya Madini nchini na matarajio ya wadau kwa ujumla.

Ujenzi huu wa maabara kubwa na ya kisasa utaenda sambamba na ujenzi wa maabara za kanda na kuwajengea uwezo watumishi wa GST ili kuendana na kasi kubwa ya maendeleo ya Teknolojia duniani.

Mh. Mavunde ameyasema hayo jana Aprili 24, 2024 jijini Dodoma katika kikao cha pamoja cha kujadili namna bora ya utendaji kazi kilichowakutanisha  Watumishi wote wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST).

“Jukumu letu la kimsingi ni kuhakikisha kwamba Taasisi hii inatoa mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya madini hapa nchini Tanzania.

Taarifa za maabara kutoka GST zinapaswa kuwa za uhakika na sahihi kwa wachimbaji,hili ni jukumu ambalo kama serikali hatuwezi kulikwepa.

Tumedhamiria kuhakikisha tunajenga maabara kubwa, ya kisasa na tegemeo katika utoaji wa huduma ndani na nje ya mipaka Tanzania”Alisema Mavunde

Waziri Mavunde ameongeza pia kuwa  GST ina mchango mkubwa katika ukuaji wa Sekta ya Madini huku akisisitiza kwamba GST ni Moyo wa Sekta ya Madini nchini, kutokana na umuhimu huo Serikali imeendelea kuiwezesha zaidi GST ili itekeleze majukumu yake kwa ufanisi unaotarajiwa.

Mavunde ametumia fursa hiyo kuwataka watumishi wote kujituma na kufanya kazi kwa weledi katika kutekeleza majukumu ya GST na kusisitiza kwamba hatakuwa tayari kumvumilia mtu yoyote ambaye hatakuwa tayari kuchapa kazi kwa bidii ili kufikia maono na matarajio ya Wizara na wadau kwa ujumla.

Pia, amesema umoja na mshikamano ndiyo kitaisaidia Taasisi hiyo kusonga mbele  na kuwataka watumishi wote kufanya kazi kama timu moja.Kwa umoja wetu utasaidia kufikia malengo tuliyojiwekea ya kufanya utafiti wa kina wa asilimia angalau 50 ifikapo mwaka 2030.

Akitoa maelezo ya awali, Katibu Mkuu wa Wizara ya Madini Ndg. Kheri Abdul Mahimbali amewaahidi watumishi wa GST kushughulikia changamoto mbalimbali za kiutumishi walizonazo ili kuboresha mazingira yao ya kufanya kazi.

Akitoa salamu za shukrani,Mtendaji Mkuu wa GST Dkt. Mussa Budeba ameishukuru serikali kwa kuipa kipaumbele Taasisi ya GST na kuahidi kusimamia utekelezaji wa maagizo yote yaliyotolewa ili kuongeza na kuboresha ufanisi wa Taasisi.

Share To:

Post A Comment: