NAIBU Waziri wa Maji Mhandisi Maryprisca Mahundi (Mb) ameiagiza Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Tabora (TUWASA) kuhakikisha wanapunguza mianya ya upotevu wa mapato na kuhakikisha wanaelekeza nguvu kwenye maeneo yote kuhakikisha wananchi wanapata maji kama ilivyo dhamira ya Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa wananchi.

Kadhalika Mhandisi Mahundi ameagiza kujengwa kwa Ofisi nzuri ya TUWASA Kaliua ,na kuagiza vijana wanaofanya kazi katika vyombo vya watoa huduma ya maji ngazi ya Jamii kupewa ajira ya miaka miwili wakati taratibu zingine za kiutumishi zikiendelea kufanyika ili wawe waajiriwa wa Wizara ya Maji.

Mahundi ameyasema hayo leo Januari 25 2024, akiwa anahitimisha ziara yake ya kikazi ya kukagua utekelezaji wa miradi ya maji Urambo na Kaliua Mkoani Tabora .

“Pamoja na mambo mengine TUWASA ongezeni mapato kwakuwa bado kuna kazi ya kufanya licha ya kuwa na mafanikio yaliyopo msiridhike na hapa mlipokia pia muwe karibu na wananchi ili kupata taarifa kwa wananchi kuhusu maji yanayopotea”amesema Mahundi

Amewataka menejimenti za TUWASA na RUWASA kutokuwa wabinafsi kwa watumishi wanaowasimamia kwa kuwapa motisha na kuheshimiana ambapo pia amewapongeza watumishi wote wa sekta ya maji Tabora kwa utendaji kazi na amewataka kuendeleza umoja, ushirikiano, upendo na kuthaminiana kama familia moja ya Wizara ya maji kwa uwajibikaji kwa wananchi.

Sambamba na hayo Mhandisi Mahundi ametoa rai kuwa vituo vya afya na shule vipewe vipaumbele katika huduma ya maji bila kusahau usafi wa mazingira kwa kuondoa majitaka na kusambaza majisafi na salama.

RUWASA imeeleza kwamba itaendelea kutekeleza miradi vijijini maeneo ambayo hayajafikiwa.

Nae Dkt.Rashid Chuachua Mkuu wa Wilaya ya Kaliua amesema Kaliua wanamshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa mpango wa utatuzi wa changamoto ya maji Kaliua huku akisema Wilaya hiyo ina watu zaidi ya laki 6 na uhitaji wa maji ni wa kiasi kikubwa zaidi.

“Naomba Wilaya hii iangaliwe kwa jicho la kipekee sana na nipende kuwapongeza Mhe. Waziri wa maji na Naibu Waziri wa maji kwa kuhakikisha wananchi wanapata maji kwani wanafanya kazi kubwa”amesema

Mhandisi Mahundi amekamilisha Ziara yake kwa kutembelea mradi wa maji wa Kata ya Maboha kijiji cha Usinge na Mitimitano ambao umekamilika na kubakisha shilingi milioni 20 ambazo ameagiza zijenge vituo nane (08) vya kuchotea maji kwa ajili ya wananchi eneo la miti mitano na Usinge.

Share To:

Post A Comment: