Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba amesema matumizi ya fedha za mapato ya ndani kupitia wataalamu wa ndani yaani “ Force Acount” katika ujenzi wa miradi mbalimbali hapa nchini sio tatizo ili tatizo ni kukosekana kwa wasimamizi makini wa miradi hiyo.

Amesema dhamira ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Awamu ya sita wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuona watanzania wanashikilia uchumi wa nchi yao wenyewe kwa kushiriki katika Nyanja zote za maendeleo ikiwemo miradi mikubwa ya ujenzi wa miundombinu na sio kutegemea wataalamu kutoka nje ya nchi na mwisho wao faida yote wanapeleka katika mataifa yao.
Dkt.Nchemba ameyasema hayo leo Machi 12,2024 Jijini Dodoma ,wakati wa hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi jengo la taaluma katika Kampasi ya Dodoma ya Chuo Cha Uhasibu (IAA) inayojengwa na chuo hicho kwa kutumia fedha za mapato yake ya ndani kupitia wataalamu wa ndani yaani “Force Account”
“Tulipoanza kutumia Force Accout watu wakaanza kupiga kelele ila niwaambie ukweli Force Account haina tatizo lolote ila tatizo ni kukosekana kwa wasimamizi makini wenye uzalendo ndio maana miradi ilikuwa inasuasua na mengine wanatekeleza chini ya kiwango ila hapa IAA wanatuonesha jinsi Force Account inavyoweza kutumika na ikaleta matokeo mazuri.
Na kuongeza kuwa “dhamira ya Dkt. Samia ni kuona watanzania wanashikilia uchumi wa nchi yao wenyewe sasa tunapokosa usimamizi mzuri katika miradi yetu na wataalamu wetu kutoshiriki katika miradi mikubwa dhamira hii nzuri ya Rais wetu itakuwa ni bure kwani Watanzania tutaendelea kuwa nyuma na wageni wataendelea kufurahia kuchuma na kupeleka maendeleo katika mataifa yao sisi huku tunabaki kuwa watazamaji wakati serikali imeweka kila aina ya jitihada za kushirikisha watanzania katika ujenzi wa uchumi wa nchi” amesema Dkt. Nchemba
Dkt.Nchemba ameuagiza uongozi wa chuo hicho kukuendelea kusimamia kwa ukaribu ujenzi wa jengo hilo na kuzingatia viwango vya ubora,sheria ,taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha za umma na kukamilisha miradi hiyo kwa wakati na kuonesha thamani halisi ya fedha.
Amesema matarajio ya Serikali katika ujenzi wa miundombinu ya elimu kama madarasa ,kumbi za mihadhara ,maktaba maabara za kompyuta unaeendelea katika kampasi zote za Chuo cha Uhasibu (IAA) zitaleta chachu katika kutoa elimu bora kwa wananchi.
“Miundombinu hii itawawezesha kuwaandaa wataalam mahiri kwenye fani za Uhasibu,Benki,Fedha ,uchumi,usimamizi wa rasilimaliwatu,ununuzi na ugavi ,usimamizi wa biashara ,utalii ,masoko na maeneo mengine watakakokidhi mahitaji ya soko la ajira wakiwa na ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumi,” ameeleza Dkt.Nchemba
Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uhasibu (IAA) Prof. Eliamani Sedoyeka amesema jengo hilo lina ghorofa sita na litakuwa na madarasa ,ofisi,maktaba, na maabara ya kompyuta ambapo likikamilika litakuwa na uwezo wa kuchukua wanafunzi 4500 kwa wakati mmoja.
Amesema katika miaka miwili ijayo Chuo hicho kinatarajia kukamilisha Jengo Kuu (Campus Main Building) ambapo litawezesha Kampasi ya Dodoma kudahili wanafunzi 7,806 kwa mwaka.
“Napenda kutoa wito kwa wanafunzi wetu watarajiwa kuchangamkia fursa ya kujiunga na Chuo chetu ili kujenga mustakabali wao kwa kujifunza na kukua kitaalamu , na tutajitahidi kufanya kila linalowezekana kuwawezesha kufikia malengo yao ya elimu na kazi,” amesema Prof. Sedoyeka
Naye Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuunga mkono Chuo hicho katika ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo katika kipindi cha miaka miwili shilingi bilioni tatu (03) zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi unaoendelea katika Kampasi ya Arusha na Kampasi ya Babati.
Aliahidi kuwa Chuo kitaendelea kusimamia matumizi ya fedha hizo na kuhakikisha kuwa zinafanya kazi iliyokusudiwa pamoja na kuhakikisha kwamba Chuo chao kinatoa wahitimu wenye weledi na ujuzi unaohitajika katika kuleta maendeleo ya taifa.
Chuo cha Uhasibu Arusha kinaendelea na ujenzi wa jengo la Taaluma litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 4,500 kwa wakati mmoja, kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) na linatarajiwa kukamilika mwezi Julai na litaanza kutumika mwezi Oktoba, 2024.
Share To:

Post A Comment: