Waziri wa Fedha Mhe. Dkt.Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), ameuagiza uongozi wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA) kusimamia kwa ukaribu ujenzi miundombinu yake inayoendelea kujengwa ili ikidhi viwango vya ubora na kuonesha thamani halisi ya fedha.
Alisema hayo wakati wa hafla ya kuweka jiwe la msingi katika jengo la Taaluma la Chuo cha Uhasibu Arusha katika Kampasi ya Dodoma, linalojengwa eneo la Njedengwa wilaya ya Dodoma, Jijini Dodoma.
Alisema ni muhimu kuzingatia usimamizi mzuri katika ujenzi wa majengo mengine ya hosteli, utawala, madarasa pamoja na kumbi za mihadhara yanayoendelea kujengwa katika Kampasi za Arusha na Babati, ili watekeleze miradi hiyo kwa kuzingatia viwango vya ubora, sheria, taratibu na miongozo ya matumizi ya fedha za umma na kukamilisha miradi hiyo kwa wakati ili iweze kutoa huduma kwa Watanzania.
‘‘Miongoni mwa malengo Endelevu ya milenia kufikia mwaka 2030 ni kila nchi kutoa Elimu bora kwa watu wake. Ninawapongeza kwa kuwa mstari wa mbele kuunga mkono jitihada za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, katika utekelezaji wa malengo ya milenia katika Sekta ya elimu,’’ alisema Dkt. Nchemba.
Aidha alisema kuwa matarajio ya Serikali kupitia ujenzi wa miundombinu ya elimu kama madarasa, kumbi za mihadhara, maktaba, maabara za kompyuta unaoendelea katika Kampasi ya Dodoma na Kampasi za Arusha, Babati utakuwa chachu katika kutoa elimu bora kwa Watanzania.
‘‘Ninaamini miundombinu hiyo itawawezesha kuwaandaa wataalam mahiri kwenye fani za Uhasibu, Fedha, Benki, Uchumi, TEHAMA, Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ununuzi na Ugavi, Usimamizi wa Biashara, Utalii, Masoko na maeneo mengine wataokakidhi mahitaji ya soko la ajira, wakiwa na ujuzi na maarifa ya kukabiliana na changamoto za kijamii na kiuchumii’’ alisema Dkt. Nchemba.
Aidha, alitoa rai kwa Chuo hicho kuendelea kubuni kozi mbalimbali ambazo zitawasaidia Watanzania kuelimika na kujikwamua kiuchumi pamoja na kufanya tafiti zitakazoleta tija kwa Taifa ambazo matokeo yake yataisaidia serikali, jamii na wadau wengine kuzitumia kama dira katika kufanya maamuzi mbalimbali yenye mchango katika ukuaji wa uchumi wa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.
Alisisitiza kuwa Wizara ya Fedha itaendelea kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha katika kuhakikisha kinatekeleza majukumu ya msingi kama Taasisi ya Elimu ya Juu ambayo ni kutoa mafunzo, kufanya tafiti na kutoa ushauri wa kitaalam.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Uongozi la Chuo Cha Uhasibu Arusha (IAA), Dkt. Mwamini Tulli, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuunga mkono Chuo hicho katika ujenzi wa miundombinu ya elimu kwa lengo la kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia ambapo katika kipindi cha miaka miwili shilingi bilioni tatu (03) zilipokelewa kwa ajili ya ujenzi unaoendelea katika Kampasi ya Arusha na Kampasi ya Babati.
Aliahidi kuwa Chuo kitaendelea kusimamia matumizi ya fedha hizo na kuhakikisha kuwa zinafanya kazi iliyokusudiwa pamoja na kuhakikisha kwamba Chuo chao kinatoa wahitimu wenye weledi na ujuzi unaohitajika katika kuleta maendeleo ya taifa.
Naye Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Eliamani Sedoyeka aliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa ajili ya fedha za mradi wa HEET ambao Chuo hicho kimetengewa kiasi cha Sh. bilioni 48 ambazo zinatarajiwa kuendelea kuboresha Chuo katika nyanja mbalimbali.
Alisema Kwa kutambua kuwa Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi, Chuo cha Uhasibu Arusha kupitia Kampasi ya Dodoma kitaendelea kutoa mafunzo ya shahada ya uzamili kwa mwaka mmoja kwa kufundisha darasani vipindi vya jioni kwa njia ya darasani na mtandao kwa pamoja , pia kinatarajia kuanza kutoa masomo ya jioni kwa baadhi ya kozi za stashahada (diploma).
Chuo cha Uhasibu Arusha kinaendelea na ujenzi wa jengo la Taaluma litakalokuwa na uwezo wa kuhudumia wanafunzi 4,500 kwa wakati mmoja, kwa kutumia mapato yake ya ndani kwa kutumia wataalam wa ndani (Force Account) na linatarajiwa kukamilika mwezi Julai na litaanza kutumika mwezi Oktoba, 2024.
Post A Comment: