Wizara ya Madini imekuwa  miongoni mwa Wizara zilizoshiriki  Kilele cha Kongamano la KURASA 365 za MAMA Vol.III. lililoratibiwa na Clouds Media Group.

Kongamano hilo limehitimishwa leo Machi 27, 2024 jijini Dar Es Salama na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa ambaye amezungumzia umuhimu wa Serikali  kuendelea kutangaza mafanikio mbalimbali yaliyofikiwa katika Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Katika Kongamano hilo, Wizara mbalimbali zimepata wasaa wa kueleza masuala makubwa yaliyofanyika katika Siku 365 za Rais Samia madarakani ikiwemo mikakati ya kuendeleza Sekta hizo.

Akizungumza katika Kongamano hilo, Naibu Waziri wa Madini  Dkt. Steven Kiruswa ameileza hadhira iliyoshiriki  kuhusu umuhimu wa Sekta ya Madini katika kuchochea uchumi na shughuli nyingine za kiuchumi hivyo kuelezea mikakati ya Serikali kuboresha miundombinu ya barabara ili kuwezesha miradi ya madini kufanyika kwa tija.

Dkt. Kiruswa  ametolea mfano  ujenzi wa barabara itakayowezesha usafirishaji wa madini katika kiwanda kikubwa na cha aina yake cha kusafisha madini ya metali yakiwemo Madini ya nikeli  kinachotarajiwa kujengwa  Wilayani Kahama Mkoa wa Shinyanga ambapo hivi karibuni Serikali ilitoa Leseni ya kiwanda hicho.

” Mikakati ya Serikali ni kuunganisha  barabara ya kwa Msisi Handeni ili kuiunganisha na barabara ya Tanga Dar Es Salaam kuweza kusafirisha Madini ya Kinywe yanayochimbwa na Mtanzania GodMwanga,” amesema Dkt. Kiruswa.

Akizungumzia ukuaji wa Sekta ya Madini, Dkt. Kiruswa amesema kumekuwa na kasi kubwa ya ukuaji wa Sekta ya Madini hali inayodhihirisha kufikiwa kwa malengo ya kufikia asilimia 10 ya mchango wa Sekta ya Madini  kwenye Pato laTaifa ifikapo Mwaka 2025  kama ilivyoanishwa katika Dira ya Maendeleo ya Taifa.

Aidha, Dkt. Kiruswa amebainisha mikakati mingine kuwa ni pamoja na  kuwaendeleza na kuwainua wachimbaji wadogo wa madini nchini ikiwemo kuweka tozo ndogo ili kuwawezesha wafanye shughuli zao kikamilifu na hivyo kuchangia mapato ya Serikali.

Share To:

Post A Comment: