Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa William Mwegoha amesema tafiti mbalimbali
zinazofanywa na wanataaluma wa chuo hicho zimelenga kuwainua vijana wa kitanzania kwa
kuwapatia mitaji kupitia uchangiaji wa umati.

Profesa Mwegoha amesema hayo Januari 24, 2023  wakati wa uzinduzi wa kongamano la Kimataifa
linalofadhiliwa na Serikali ya Denmark kupitia mpango wa kutumia michango ya umati kwenye
kuwezesha wajasiriamali wadogo nchini Tanzania (C4YET ) lililofanyika Jijini Arusha.

Amesema tafiti hizo zimelenga kuangalia mbinu mbalimbali, faida kwa mlengwa na faida kwa
mchangiaji  ili kuwainua vijana na wajasiriamali wadogo wadogo kupitia uchangiaji wa umati.

“Kwa chuo chetu Mzumbe ni utafiti wenye manufaa makubwa kwasababu unachangia sana kwenye
dhana ya Serikali ya kuhakikisha wajasiriamali wadogo wanawezeshwa mitaji” amesema Prof.
Mwegoha.

Amesema kupitia kongamano hilo linalowakutanisha watalaamu kutoka vyuo mbalimbali ikiwemo
Chuo Kikuu Mzumbe na Chuo cha Copenhagen kutoka Denmark, watafiti watabadilishana matokeo
ya utafiti na kupata njia sahihi yakutekeleza dhana ya uchangiaji wa umati.

Profesa Mwegoha amesema mradi huo ulianza mwaka 2019 na ni wa miaka mitano ambao
umewanufaisha vijana wa maeneo yote ya mijini na vijijini.

Naye Mratibu wa mradi huo,Dkt. Nsubili Isaga kutoka skuli ya biashara Chuo Kikuu Mzumbe
amesema mradi huo umewainua wajasiriamali kutokana na kubuni nyenzo walizotumia za uandishi
wa andiko lililowavutia wafadhili kwaajili ya wanataaluma kusaidia tafiti na hatimaye chuo hicho
kushirikisha SIDO kwaajili ya kuwakwamua wajasiriamali vijana kwenye mikoa mitano ambayo ni
Arusha, Mwanza, Dar es Salaam, Morogoro na Mbeya.

Ameongeza  kuwa jumla ya wajasiriamali 187 walipewa mafunzo hayo ambapo wajasiriamali 100 kati
yao waliweza kupata mikopo yenye riba ya asilimia 5 tu inayowawezesha wao kurejesha mikopo yao
kwa wakati na baadae vijana wengine watafikiwa zaidi ili wajiunge na majukwaa ya biashara
mitandaoni

Share To:

Post A Comment: