WAZIRI wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa,akizungumza na Waandishi wa habari leo Septemba 7,2023 jijini Dodoma mara baada ya kukutana na Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakati wa ziara yake katika taasisi hiyo tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.



WAZIRI wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa,akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro,wakati wa ziara yake ya kukutana na Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) leo Septemba 7,2023 jijini Dodoma tangu alipoteuliwa kuwa Waziri wa Ujenzi.



Sehemu ya Menejimenti ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wakimsikiliza Waziri wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa (hayupo pichani) wakati wa Kikao kilichofanyika leo Septemba 7,2023 Makao Makuu ya TBA jijini Dodoma.


............................

WAZIRI wa Ujenzi, Mhe. Innocent Bashungwa, ameuagiza Wakala wa Majengo (TBA), kuhakikisha unakusanya deni la Shilingi Bilioni 81.5 wanazodai kwa wapangaji wao sambamba na kuwaondoa wadaiwa sugu katika nyumba hizo ili upatikanaji wa fedha hizo uweze kusaidia utekelezaji wa miradi mingine nchini.

Waziri Bashungwa ameyasema hayo leo Septemba 07, 2023 jijini Dodoma mara baada ya kufanya ziara yake katika Wakala huo na kuzungumza na menejimenti ya TBA ambapo amesisitiza uwekezaji wenye tija kwa watumishi na Taifa kwa ujumla.

“TBA simamieni sheria kwa yeyote asiyelipa kodi hata kama ni kiongozi, waandikieni notisi ya kulipa madeni yao na wasipolipa waondoeeni, wapo wengine nje wanasubiri wapewe nyumba ili waweze kulipa kodi kwa wakati na tutamia makusanya hayo kujenga nyumba nyingine”, amesema Mhe.Bashungwa.

Aidha, Bashungwa ameagiza TBA kuhakikisha wanakuja na mikakati itakayosaidia kujenga nyumba za bei nafuu hasa kwa vijana wanaoajiriwa katika utumishi wa umma hususan Dodoma ili kuweza kumudu gharama za maisha.

“Kuna vijana ambao wanaingia kwenye kada ya utumishi wa umma na bado hawajawa na uwezo wa kujijengea nyumba, kupitia TBA mnaweza kujenga nyumba za bei rahisi kwa ajili ya vijana hao ili kuwarahisishia gharama za Maisha”, ameeleza Bashungwa.

Hata hivyo Waziri Bashungwa ameutaka Wakala huo kuwa na utaratibu wa kuwajengea uwezo wataalamu walionao ili kuenda sambamba na kasi ya mabadiliko ya teknolojia hasa katika suala la ujenzi na uendelezaji wa majengo mbalimbali.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud Kondoro, amesema kuwa watahakikisha wanatafuta ufumbuzi wa changamoto zilizopo na kumuahidi Waziri Bashungwa kuandaa mikakati mizuri itakayosaidia Wakala huo kutoa huduma bora kwa wananchi.

Awali akitoa taarifa, Arch. Kondoro amesema kuwa hadi sasa TBA inaendelea kutekeleza mradi wa ujenzi wa nyumba 3500 za watumishi wa umma eneo la Nzuguni Dodoma ambapo awamu ya kwanza ya nyumba 150 utekelezaji umefikia asilimia 95 na awamu ya pili ya ujenzi wa nyumba 150 utekelezaji wake umefikia asilimia 10.

''Miradi mingine ni ujenzi wa nyumba 20 za Viongozi jijini Dodoma ambazo zililenga kukabiliana na uhaba wa nyumba za Viongozi baada ya Serikali kuhamia Dodoma ambapo mradi huo umekamilika kwa asilimia 100 na nyumba zimeanza kutumiwa na Viongozi.''amesema
Share To:

Post A Comment: