Afisa Biashara kutoka Ubalozi wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Nchini Bw. Marcel Kasongo Yampanya amewasilisha nia ya Serikali ya Kongo kuleta Vijana wengi nchini Tanzania kujifunza Uongezaji Thamani wa Madini ya Vito katika Kituo cha Jemolojia Tanzania (TGC) cha jijini Arusha.

Ameyabainisha  hayo  wakati wa mazungumzo yake na viongozi wa kituo cha TGC baada ya kukitembelea  Septemba 19, 2023 katika ziara iliyolenga kujifunza na kuona namna ya kushirikiana na kituo hicho katika masuala ya Uongezaji Thamani Madini ya Vito  pamoja na kuhakikisha ushirikiano wa karibu kati ya nchi hizo mbili katika kukuza sekta hiyo ndogo.

Ziara hiyo  inakuja wakati ambapo  nchi ya Kongo imeonyesha nia ya kukuza sekta ya madini ya vito na kuleta vijana wa Kongo kujifunza kutoka kwa wataalam  wa Tanzania ambao wamekuwa wakiongoza katika  utoaji wa mafunzo ya uongezaji thamani wa madini ya vito kwa upande wa Afrika ya Mashariki na Kati.

Aidha, sehemu kubwa ya wakufunzi wa kituo hicho tayari wamepata utaalam wa shughuli hizo kutoka nchi mbalimbali zilizoendelea katika eneo hilo ikiwemo Thailand, India na China.

Aidha, ziara hiyo ya Afisa biashara wa Kongo imekuja ikiwa zimepita siku chache tu baada ya ujumbe wa Tanzania kutembelea shughuli za uongezaji thamani madini katika viwanda vikubwa, vya kati na vidogo nchini Thailand ambapo shughuli hizo zimeshamiri kwa kiasi kikubwa. Katika ziara hiyo, Mratibu wa Kituo hicho pia alikuwa sehemu ya ujumbe huo.

Katika ziara ya hivi karibuni  nchini  Thailand, Wizara ya Madini kupitia kituo hicho ilifanya mazungumzo  na taasisi kadhaa kuhusu  namna ya kushirikiana na kubadilishana uzoefu katika masuala ya uongezaji thamani  ikiwemo  kiwanda kikubwa chenye uzoefu wa miaka 50 katika  shughuli za uongezaji thamani madini ambapo wadau nchini humo walifungua milango kwa watanzania  kujifunza ili kuwa bora katika eneo hilo.

Katika kikao hicho, Kaimu Mratibu wa TGC Bw. Daniel Kidesheni amepokea ahadi ya balozi na kuahidi kuendeleza ushirikiano mzuri kati ya taasisi hizo mbili. Amesisitiza umuhimu wa kubadilishana uzoefu na kuendeleza teknolojia za kisasa ili kuhakikisha kuwa sekta  ndogo ya madini ya vito inachangia  katika ukuaji wa uchumi na maendeleo katika nchi hizo.

Katika ziara hiyo,  Bw. Kasongo  amepata fursa ya kutembelea karakana mbalimbali za TGC, ikiwa ni pamoja na maabara za kisasa zinazotumika kwa uchunguzi wa madini ya vito, usonara na ukuataji na ung’arishaji wa madini ya Vito.

Ziara hiyo ya Afisa biashara kutoka ubalozi wa Kongo nchini Tanzania imekuwa hatua muhimu katika kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika sekta ndogo ya madini ya vito.Share To:

Post A Comment: