Na Immanuel Msumba; Monduli

Siku moja kabla ya jua kuchomoza, Lilian Mollel, mama wa watoto watatu kutoka Kijiji cha Lepruko, anachukua ndoo na kuanza safari ndefu ya kilomita 20 kutafuta maji. Hii ni kawaida kwa wanawake wa jamii ya Kimaasai huko Monduli. Zaidi ya vijiji 50 vinavyokaliwa na jamii hii vimeathirika vibaya na uhaba wa maji kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Jamii ya Kimaasai, inayojulikana kwa utamaduni wake wa kipekee wa ufugaji, lina historia ndefu na tamaduni zinazoendelea hadi leo. Wakiwa wameenea katika Nchi za Tanzania na Kenya, wamekuwa wakilinda utamaduni wao wa karne nyingi ambapo wamekuwa wakijikita katika ufugaji wa Ngombe, Kondoo na Mbuzi.

Uhamahama wao kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo yao umeleta matokeo yasiyotarajiwa kwenye vyanzo vya maji katika maeneo yao ya makazi, hasa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

Monduli ni moja ya wilaya sita za Mkoa wa Arusha nchini Tanzania, iko kaskazini- mashariki mwa nchi na ina wakazi takribani 227,585 (sensa ya 2022). Wilaya hii inajumuisha kata 8 na ina eneo la jumla la kilomita za mraba 6,419, ambapo 6290.62 km^2 ni ardhi na 128.38 km^2 ni maji. Milima kama Monduli, Lepurko, na Loosimingori inaipa wilaya tabia ya kipekee ya topografia. Monduli ni kati ya wilaya kavu zaidi Tanzania, tatizo la maji limekuwa linaloongezeka kwa kasi na kuwaathiri wakazi wake.

Kulingana na takwimu kutoka Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), wilaya hiyo ina vyanzo 64 vya maji, ambapo 61 kati yake vimekauka katika kipindi cha mwaka jana pekee kutokana na ukame uliotokana na mabadiliko ya tabianchi. Hii inamaanisha kuwa asilimia 95 ya vyanzo hivyo vya maji vimepotea, na kuiacha jamii hiyo katika hali ya shida kubwa.

Hii siyo tu takwimu. Kwa wanawake kama Lilian Mollel, hii ina maana ya kuongezeka kwa mzigo wa kila siku wa kutafuta maji kwa familia zao. Uhaba huu wa maji unamaanisha kuwa wanawake wengi wanatumia saa nne hadi tano kila siku kutembea kwenda na kurudi kutoka kwenye vyanzo vya maji vilivyobaki. Kwa wastani, hii ni sawa na kutembea kwa kilomita 15 hadi 20 kila siku.

Zaidi ya hiyo, safari hizi za kutafuta maji zimekuwa na hatari zake. Wanawake na watoto, ambao mara nyingi ndio wanaopewa jukumu la kutafuta maji, wanakabiliwa na tishio la wanyama wakali kama simba, tembo, na fisi. Hali hii pia inaongeza hatari ya matukio ya kiusalama kama vile ubakaji.

Wanawake hawa wa jamii ya kimaasai wanakusanyika pamoja na watoto ili kutengeneza kundi kubwa kwa ajili ya kuamshana saa tisa usiku kufuata maji kutokana na wanaume wa familia hizo kuwa mbali na kwa ajili ya Kwenda kutafuta maeneo ya malisho ya mifugo yao.

Katika familia ya Saitabahu Mollel ambaye yupo Simanjiro Mkoani Manyara kwa ajili ya kutafuta malisho ya mifugo mkewe Lilian Mollel anatueleza kuwa katika jamii  anayoishi ya Kijiji cha Lepruko amekuwa akikabiliwa na janga la maji ambalo limekuwa kero sugu katika Kijiji chao jambo ambalo linamzuia kuweza kufanya shughuli nyingine za kimaendeleo.

"Mateso haya yametufanya tuone kuoga kila siku ni anasa badala yake tunaoga mara moja kwa wiki, lakini hali hii inatuweka katika hofu kubwa ya magonjwa ya mlipuko maana juzi tu nimesikia huko Arusha nako kuna kipindupindu, lakini zaidi baa la njaa kutokana na upungufu wa chakula ulipo katika Kijiji chetu kama unavyoona mazao hayakukomaa yamekauka" Alisema Lilian

Lilian ameenda mbali na kusema kuwa kwa taarifa nilizozisikia kwenye kikao cha Kijiji ni kwamba katika wilaya ya Monduli kuna kuna zaidi ya vyanzo vya maji 64, huku 61 vikikauka kutokana na ukame na mabadiliko ya tabia nchi ambapo yamebaki mabwawa matatu pekee ambayo nayo yako hatarini kukauka kutokana na kuzidiwa uwezo wa matumizi lakini udongo kujaa kutokana na mvua zilizonyesha mwezi uliopita.

“Serikali ya Awamu ya sita inaendelea na kampeni ya kumtua mama ndoo kichwani tunamuomba Mama Samia aangalie namna bora ya kutusaidia sisi wanawake wa jamii ya kimaasai kwa kweli tunateseka sana kwa kukosa huduma ya maji safi na salama” Aliongezea Lilian

Uhaba huo wa maji unapelekea wanawake hawa wa jamii ya kimaasai kutembea umbali mrefu ilikupata maji kwaajili ya matumizi ya watoto na familia zao ukilinganisha wako peke yao nyumbani huku waume zao wakiwa katika malisho kuhakikisha mifugo haifii kwa njaa wala ukame.

Hata hivyo utafutaji huo wa maji hauwakatishi tamaa kwasababu maji ni uhai jamii hii hulazimika hata kwenda vijiji vya nje ya Wilaya hiyo ilikuweza kupata maji kama vilewanaume wao wakimasai wanavyohama hama na mifugo yao ili kupata malisho ndivyo wanawake wa jamii hiyo uhangaika kupata maji.

Inafaa kutambua kuwa kama vile makundi mengine ya kikabila,jamii ya Maasai inakabiliwa na mabadiliko ya kisasa na changamoto za kuhifadhi utamaduni wao wakati wakiendelea kuishi katika ulimwengu wa kisasa.Utamaduni wao wa kipekee na mila zimekuwa zikisilimika kutoka kizazi hadi kizazi,na juhudi zinafanyika ili kuhakikisha kuwa utamaduni wa Maasai unaendelea kuishi.

Kwa upande wake Meneja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA), Neville Msaki amesema kuwa wameliona tatizo hilo linalowatesa wakina Wanawake wa Jamii ya Kimaasai na Watoto na wameanza kufanya tadhimini ambapo wamegundua vijiji nane ndio waathirika wakubwa kutokana na vyanzo vyao vyote vya karibu kukauka, ambapo tuliomba fedha Serikali kuu ili kutekeleza mpango wa maji katika eneo hilo.
Share To:

Post A Comment: