Kila mara tunaposikia kuhusu afya na mazingira, akili zetu mara nyingi huwazia hewa safi, maji yasiyochafuliwa, na mazingira yasiyo na takataka. Lakini kwa baadhi ya jamii, kufikia viwango hivi vya afya ya mazingira ni ndoto tu, huku wakikabiliwa na changamoto ambazo nyingi huja na madhara makubwa ya kiafya. 

Fikiria maisha ambapo kila siku kuna hatari ya kupata magonjwa kutokana na kunywa maji yale yale ambayo mifugo na binadamu wameyachafua. Fikiria kuishi katika mazingira ambapo maji - rasilimali muhimu kwa maisha - yanaonekana kuwa adui badala ya rafiki. Hii ndiyo hali ya maisha kwa wakazi wa kata ya Sepeko, Wilayani Monduli.

Kata ya Sepeko Wilayani Monduli ni mojawapo ya maeneo hayo ambapo kila tone la maji lina simulizi yake, simulizi ambayo mara nyingi inahusiana na changamoto za kiafya na kusaka suluhisho. Katika jitihada za kuelewa kwa undani changamoto zinazowakabili wananchi wa Sepeko, mwandishi alisafiri umbali wa kilomita 45 kutoka Arusha Mjini kufika katika kata hiyo. 

Kata ya Sepeko, yenye idadi ya wakazi inayokaribia 13,633 kulingana na ripoti ya sensa na makazi ya mwaka 2022. Je, wananchi wa Sepeko wanaishi vipi katika mazingira kama haya, na nini kifanyike ili kubadilisha hali hii?

Kulingana na ripoti mbalimbali za kimataifa, ukosefu wa maji safi na salama ni mojawapo ya changamoto kuu zinazokumba mataifa mengi, haswa katika nchi zinazoendelea. Shirika la Afya Duniani (WHO) linakadiria kuwa zaidi ya watu bilioni moja duniani hawana upatikanaji wa maji safi na salama ya kunywa. Ukosefu huu unachangia vifo vya maelfu ya watu kila mwaka, haswa watoto, kutokana na magonjwa yanayosababishwa na maji yasiyo safi. 

Katika maeneo mengi ya dunia, upatikanaji wa maji safi na salama huwa ni haki msingi ya kila binadamu. Lakini kwa wakazi wa Sepeko, haki hii inaonekana kuwa ndoto isiyotimia. Changamoto ya maji inayowakumba ina athari mbaya sio tu kwa afya yao bali pia kwa maisha yao ya kila siku.

Kwanza kabisa, maji yao ya matumizi ya kila siku yanatoka katika mabwawa ambayo pia hutumiwa na mifugo. Uwepo wa mifugo katika vyanzo hivi vya maji unachangia uchafuzi wa maji, ambao unaweza kusababisha magonjwa ya mlipuko.

Hali hii inawaweka katika hatari kubwa ya kuambukizwa magonjwa. Baba Noel, mmoja wa wakazi wa Sepeko anaelezea, 

"Sisi tumeshazoea hatuna la kufanya ngo'ombe, Mbwa, mbuzi na pengine wanakojoa humohumo, wakiingia ndani ya bwawa kunywa maji na sisi tunachota hayohayo, hatujawahi kuugua Wala Nini, sisi hata tukipata hata hayo Maji angalau yawe masafi sio lazima yawe salama tutashukuru."

Wakazi wengine pia wanaogelea katika mabwawa hayo, wakiosha mwili wao kwa sabuni, hali inayoongeza kiwango cha uchafuzi wa maji. Neema Lemburis, mwanakijiji mwingine, anasema, 

"Kwanza sio mifugo tu kuna watu wanaogelea mtu anazama ndani na sabuni anaoga humohumo na tunachota hatuchemshi wala nini mungu pekee anatulinda."

Changamoto hii ina athari kubwa kwa afya ya jamii, hasa watoto na wazee ambao huwa hatarini zaidi kuambukizwa magonjwa. Pamoja na hatari za kiafya, ukosefu wa maji safi na salama pia unaweka shinikizo kubwa kwa wanawake na wasichana ambao mara nyingi ndio wanaopewa jukumu la kuchota maji kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Viongozi wa serikali ya kijiji cha Sepeko hawakuficha ukweli wa shida ya maji inayowakabili wananchi wao. Walikiri wazi kuwa, licha ya jitihada mbalimbali,wananchi wa kata hiyo, kama ilivyo kwa wilaya nzima ya Monduli, wanakabiliwa na changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji safi na salama. 

Wakaazi wa Sepeko wanategemea sana mabwawa ambayo mara nyingi yamechanganyikana na maji yaliyochafuka, hatua inayowaacha wazi kwa magonjwa ya milipuko.

Changamoto ya upatikanaji wa maji safi na salama katika kata ya Sepeko haikuanza juzi. Hii ni hali ambayo imekua ikiwaathiri wananchi wa eneo hili kwa muda mrefu.

Licha ya jitihada mbalimbali za kuboresha hali hiyo, bado changamoto hii imeendelea kuwa kikwazo kikubwa katika maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika kata hiyo.

Sababu kuu inayochangia ukosefu wa maji katika eneo hili ni kuongezeka kwa ukame, ambao kwa kiasi kikubwa umefanikishwa na mabadiliko ya tabia nchi.

Mabadiliko haya yamesababisha kupungua kwa mvua katika eneo la Sepeko, hali ambayo imeathiri vyanzo vya maji kama vile mito, mabwawa, na visima. Kwa kuongezea, mabadiliko ya tabianchi yameongeza joto katika eneo hilo, kusababisha kuongezeka kwa kiwango cha uvukizaji wa maji kutoka kwenye vyanzo hivyo.

Mapendekezo ya Kuboresha Hali ya Upatikanaji wa Maji Safi na Salama:

1. Ujenzi wa Miundombinu Bora ya Maji: Kuna haja ya kuanzisha miradi mipya ya maji safi na salama katika eneo la Sepeko. Hii inaweza kujumuisha ujenzi wa mabomba ya maji kutoka vyanzo visafi, visima virefu, na hata mabwawa mapya yaliyotengwa kwa matumizi ya binadamu pekee.

2. Ushirikiano na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali: Serikali inapaswa kushirikiana kwa karibu na mashirika yasiyo ya kiserikali yanayojihusisha na masuala ya maji na mazingira ili kufanikisha miradi mipya na kubwa zaidi ya maji.

3. Mafunzo ya Ujuzi kwa Jamii: Wakazi wa Sepeko wanapaswa kupata mafunzo endelevu kuhusu mbinu za kisasa za kutunza, kuhifadhi, na kutumia maji kwa ufanisi. Elimu hii itawapa ujuzi wa kuepuka matumizi mabaya ya maji na kuhakikisha kuwa maji yaliyopo yanatumika kwa ufanisi mkubwa.

4. Kuboresha Usafi wa Vyanzo vya Maji: Kuna umuhimu wa kufanya jitihada za ziada katika kuhakikisha vyanzo vya maji vinabaki safi. Hii inaweza kujumuisha kuanzisha timu za usafi wa mazingira ambazo zitakuwa na jukumu la kuhakikisha vyanzo hivyo vinabaki visafi kwa wakati wote.

5. Uanzishwaji wa Miradi ya Maji ya Mvua: Kwa kutumia teknolojia za kisasa, wananchi wa Sepeko wanaweza kuanzisha miradi ya kukusanya maji ya mvua. Maji haya yanaweza kutumika kwa matumizi mbalimbali, haswa wakati wa vipindi vya kiangazi.

6. Kuhamasisha Uwekezaji katika Sekta ya Maji: Serikali inapaswa kuweka mazingira mazuri ya uwekezaji katika sekta ya maji, ikiwa ni pamoja na kutoa vivutio kwa wawekezaji wanaotaka kuanzisha miradi ya maji katika maeneo kama Sepeko.

7. Mikakati ya Ufuatiliaji na Tathmini: Baada ya kutekeleza miradi mbalimbali, kuna haja ya kuwa na mikakati madhubuti ya kufuatilia na kutathmini matokeo ili kuhakikisha kwamba malengo ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama yanafikiwa.
Share To:

Post A Comment: