Chuo cha Uhasibu Arusha IAA kwa kushirikiana na Jeshi la magereza nchini wamezindua programu ya mafunzo  ya elimu na ufundi stadi ya muda mfupi kwa wafungwa  wanaokaribia kumaliza muda wao wa kutumikia kifungo, leo katika gereza la Kisongo Jijini Arusha. 

Akizindua mafunzo hayo  Mkuu wa Jeshi la Magereza Nchini ACP. Jeremiah Yoram Katungu amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Samia Suluhu Hassan kwa kuunda Tume haki jinai inayolenga kuleta ufanisi  katika kurekebisha wafungwa kwa kuwapa elimu ya stadi za maisha na biashara ili waweze kujitegemea pindi watakaporejea katika jamii zao baada ya kumaliza muda wa kutumikia kifungo. 

Amepongeza uongozi imara uliotukuka wa awamu ya sita uliopelekea nchi kupiga hatua kubwa katika nyanja mbalimbali sambamba na kuliwezesha jeshi la magereza kutekeleza maelekezo ya majukumu yake kwa ufanisi na weledi. 

"Nimeyaona mafanikio makubwa tangu tulipotiliana saini ya makubaliano haya Jijini Dar es salaam, naahidi kwamba tutashirikiana kwa karibu kuhakikisha tunatimiza adhma yetu ya kuwaona wafungwa wanapata ujuzi wa biashara, ufundi na ujasiriamali baada ya kumaliza muda wao wa kifungo"amesema ACP Katungu. 

Ameongeza kwamba tayari wameandaa mitaala mahususi na kuwapatia elimu maofisa wa jeshi la magereza watakatoa mafunzo ya elimu hiyo kwa ufanisi, na kuongeza kuwa hadi sasa Wafungwa 201 nchi nzima tayari wamepatiwa vyeti na VETA baada ya kupata ujuzi wakiwa gerezani. 

Pia ACP Katungu ametoa rai kwa wafungwa 40 wakiwemo  wanaume 30 na wanawake 10 ambao wamekuwa wa kwanza kwa gereza la Arusha kupata mafunzo hayo kuwa chachu kwa wengine na kuleta mabadiliko chanya yanayolenga mafunzo hayo kutolewa katika magereza yote nchini. 

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha IAA Prof. Eliamani Sedoyeka amesema wajibu wao ni kutoa mafunzo mbalimbali kwa ngazi mbalimbali kama jeshi la  magereza linavyofanya urekebu, amesema watashirikiana kutoa mafunzo yatakayofanya wafungwa wasirudie makosa pindi watapoungana na familia  zao. 

Hata hivyo ameelezea  kuwa, lengo lao ni kuona wafungwa wanapokuwa gerezani wanabadilika na kujutia makosa yao, 

na kuhakikisha hawarudii makosa yaleyale pindi watakaporejea katika familia zao, na kuwataka kuzingatia ujuzi watakaoupata ili uwafae  maishani mwao. 

"Tayari tumeshaanza kwa chuo cha magereza Dar es salaam na tunao wanafunzi 100 wa ngazi ya shahada ya pili shahada ya kwanza na stashahada, hivyo katika mwanzo huu mzuri tulioanza leo lengo ni kutoa kozi za muda mrefu za shahada ya pili, ya kwanza na astashahada kwa wafungwa wote nchini" amesisitiza Prof. Sedoyeka. 

Awali akimkaribisha mgeni rasmi Kamishna wa sheria na usimamizi wa magereza nchini CP. Nicodemas Tenga amewapongeza chuo cha uhasibu Arusha IAA kwa kuandaa mafunzo yenye Ithibati ya mtaala unaokubalika na mamlaka kidunia, ambapo kama mafunzo hayo yangelipiwa kila mmoja angetoa shilingi milioni moja. 

"Tutaendelea kuzingatia na kufanyia kazi kwa uaminifu mkubwa utekelezaji wa mapendekezo ya taasisi ya tume ya haki jinai iliyoundwa na Mh. Rais Samia Suluhu Hassan, kwa lengo la kuwanoa wafungwa na kuwaongezea thamani katika jamii zao" ameeleza CP Tenga. 

Vile vile Mkuu wa uongozi na usimamizi katika Chuo cha uhasibu  Arusha IAA Dkt. Adonijahi Abayo amebainisha namna kumekuwa na tabia ya wafungwa kurudia makosa yaleyale na kurudishwa magereza kutokana na ugumu wa maisha, hivyo mafunzo hayo yatakuwa chachu kwa kila mfungwa na kumfungulia mwanga wa maisha ya hapo baadae. 

"Tanzania kama taifa linaloendelea tuna tatizo la ajira lakini endapo wafungwa watapatiwa ujuzi wanaweza kuwa na fulsa ya kujipatia kipato kupitia ufundi ujenzi, udereva, useremala na fani nyinginezo" amesema Dkt. Abayo. 

Share To:

Post A Comment: