Na John Walter-Mbulu

Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom (HIHS) iliyopo kata ya Haydom wilaya ya Mbulu mkoani Manyara,  imefanya mahafali ya 38 ambapo jumla ya Wanafunzi 214 wamehitimu,  kati yao wavulana ni 108 na wasichana 106.

Wanafunzi hao waliohitimu, 90 ni wa taaluma ya  Uuguzi na Ukunga, huku 85 wakiwa ni tabibu na 38 Maabara.

Akitoa taarifa ,Mkuu wa chuo Bartholomayo Madangi, amesema chuo hicho  kilizinduliwa na Rais wa kwanza wa Tanzania Hayati Babati wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere 15.9.1984 na hadi leo kina mafanikio makubwa ikiwemo kutoa wataalamu wenye sifa ambao wameenea maeneo mbalimbali nchini na hata nje ya nchi.

Amewataka wahitimu hao wakafanye kazi Kwa maadili mema waliyofundishwa chuoni hapo kwa kipindi chote cha miaka mitatu na kuepuka yatakayowaharibia sifa za taaluma hiyo Muhimu.

Madangi amewaasa wazazi na walezi  kuwapeleka watoto wao katika chuo hicho ili waweze kupata elimu bora itakayo wasaidia wao kujiajiri na kumudu kwenye soko la ushindani.

Mkurugenzi wa Hospitali ya Kilutheri ya Haydom Dr. Pascal Mdoe, amesema wanaopata Mafunzo katika taasisi hiyo wana mchango mkubwa katika hospitali hiyo kwani wengi wao huajiriwa hapo kutokana na ubora baada ya kuhitimu katika chuo hicho.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi mtendaji Arusha Lutheran Medical Centre (ALMC) Dr.Goodwill Kivuyo aliyemwakilisha  Askofu  wa KKKT dayosisi ya Kaskazini kati Dkt.Solomon Massangwa, ameupongeza uongozi wa chuo hicho kwa kuwasimamia vyema wanafunzi hao ambao wanatarajiwa kuwasaidia wananchi.

Kwa niaba ya wazazi, Mwenyekiti wa UWT Wilaya ya Mbulu Yasinta Bura amewasisitiza wahitimu kuendeleza maadili mema waliyofundishwa na wakufunzi wao chuoni hapo.

Wahitimu katika risala yao wanakiri chuo hicho kimewajenga vyema na wapo tayari kukabiliana na changamoto mpya nje ya chuo.

Wahitimu katika Taasisi ya Mafunzo ya Sayansi za Afya Haydom.

Share To:

Post A Comment: