OR- TAMISEMI, Bunda


Naibu Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa anayeshughulikia Afya Dkt. Wilson Charles  Mahera amemuagiza Mkaguzi wa Ndani wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kuwasilisha ofisini kwake taarifa ya ukaguzi wa ndani ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Bunda mkoani Mara.

Dkt.Mahera ametoa agizo hilo leo katika ziara yake ya siku tatu mkoani humo kwenye ukaguzi na vikao na watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda na Halmashauri ya Mji wa Bunda.

“Ninatoa wiki mbili taarifa ya ukaguzi wa ndani ya hospitali hii ifike mezani kwangu ili kujiridhisha kuhusu matumizi ya fedha za ujenzi wa hospitali hii  na hususan zilizoletwa katika awamu ya kwanza ya ujenzi huu,” amesema Dkt. Mahera. 

Dkt. Mahera ameeleza kuwa taarifa ya ukaguzi itatoa mwanga wa yaliyofanyika wakati wa ujenzi wa Hospitali hiyo ili kama kulikuwa na ubadhirifu au ukiukaji wa maadili ya utumishi wa umma wahusika wafuatiliwa na Serikali. 

Amemuagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Bunda kuendelea kufuatilia kwa ukaribu kesi ya vifaa vya hospitali iliyopo katika Jeshi la Polisi ili wahusika waweze kuchukuliwa hatua ikiwa ni pamoja na kurejesha vifaa hivyo vyenye thamani ya shilingi milioni 56. 

Aidha, Dkt. Mahera amemtaka Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Bunda kufanya usimamizi wa karibu zaidi katika ujenzi wa hospitali hiyo ili kurekebisha mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika usimamizi wa ujenzi wa hospitali hiyo.  

Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI ameagiza pia kufufuliwa kwa kamati za ujenzi wa hospitali hiyo kulingana na mwongozo wa force account ili kuendelea kusimamia mradi huo kama ilivyokuwa awali kabla hazijaacha kufanyakazi ya usimamizi.  

Wakati huo huo, Dkt. Mahera amepongeza ubora wa majengo yaliyojengwa katika Hospitali ya Wilaya ya Bunda pamoja na ujazaji wa taarifa za masuala ya chanjo katika hospitali hiyo. 

Dkt. Mahera amewataka Waganga Wakuu wa Halmashauri kuhakikisha wanafunga mfumo wa kukusanyia mapato wa GOTHOMIS katika vituo vyote vya Serikali vya kutolea huduma za afya katika maeneo yao. 

“Kila kituo cha kutolea huduma za afya kiwe na angalau kompyuta sita na kifungwe mfumo wa GOtHOMIS ifikapo Juni, 2023 ili kudhibiti upotevu wa mapato ya Halmashauri,” amesema Dkt. Mahera. 

Kadhalika akiwa Hospitali ya Mji wa Bunda,  Dkt. Mahera ameipongeza Halmashauri hiyo kwa ujenzi wa majengo matatu yaliyo katika hatua mbalimbali na kuitaka Halmashauri kufuata mwongozo wa force account katika utekelezaji wa ujenzi huo. 

Katika Hospitali ya Manyamanyama Dkt. Mahera amezungumza na timu ya wataalamu kutoka Wizara ya Afya wanaofanya ukaguzi na mafunzo kazini kwa watumishi Mkoani Mara ili kupata mrejesho wa mambo waliyoyabaini katika uwepo wao katika Mkoa wa Mara katika kipindi cha wiki tatu walizokaa katika Hospitali hiyo na Kituo cha Afya Nyasho kilichopo katika Manispaa ya Musoma. 

Dkt. Mahera anaendelea na ziara yake kukagua miundombinu ya afya inayojengwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Rorya, Halmashauri ya Mji wa Tarime na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime. 

Share To:

Post A Comment: