Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Jumuiya ya wazazi kupitia chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini imekemea suala la ukatili ikiwemo ubakaji na ulawiti kwa watoto huku ikiziomba mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa watu wanaobainika kufanya vitendo hivyo.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti  wa Jumuiya ya Wazazi  Wilaya ya Shinyanga mjini Bwana  Fue Mrindoko kwenye ziara ya kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya ya wazazi kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga ambapo pamoja na mambo mengine amekemea suala la ukatili kwa watoto.

Mwenyekiti huyo ameiomba jamii hasa wazazi kushirikiana katika kutokomeza vitendo vya ukatili ambapo ameziomba mamlaka kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaobainika kufanya vitendo vya ubakaji na ulawiti kwa watoto na kwamba hali hiyo inachangia mmomonyoko wa maadili kwenye jamii na Taifa kwa ujumla.

“Mambo ya kunajisi watoto, mambo ya kulawiti watoto ni jambo ambalo tunalikemea sana hatulihitaji hilo na sisi kama wazazi hilo ni suala la kulihubiri kila mtu kwamba watoto wetu hawa wanaochezewa wale ambao wanahusika na vitendo hivyo wachukuliwe hatua mara moja kama wazazi tusiukumbatie uovu huo”.amesema Mwenyekiti Mrindoko

Katika hatua nyingine Mwenyekiti huyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuleta fedha nyingi kwa ajili ya maendeleo.


“Katika ziara hii tumeshuhudia miradi ya maendeleo inaendelea kutekelezwa mfano hata hili daraja linalounganisha kata ya Ibinzamata na Kitangiri ujenzi wake unaendelea vizuri na tunatarajia hadi ifikapo Juni 1,2023 daraja hili ambalo limekuwa kero kwa muda mrefu litaanza kutumika”,amesema Mrindoko.

“Ujenzi wa daraja la Kitangili unaridhisha na mwezi Juni wananchi wataanza kupita pale. Mradi huu unaendelea vizuri”,amesema.

Kwa upande wake mjumbe wa kamati ya utekelezaji jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini Mhandisi James Jumbe amesisitiza jamii hasa wazazi kuepukana na mazingira yanayosababisha ukatili kwa watoto ili kuimarisha usalama wao.

Katibu wa jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini Bi. Doris Kibabi amesema ni wajibu wa kila mzazi au mlezi kutekeleza wajibu wake wa mtoto katika malezi bora ili kuandaa Taifa bora la vijana wasomi.

Aidha katibu huyo amesisitiza matawi yote kwenye kata jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini kuongeza wanachama wapya ili kuendelea kuimarisha jumuiya hiyo.

Kamati ya utekelezaji jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini leo Mei 12,2023 imeendelea na ziara yake ya kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya kwenye kata ambapo leo pamoja na mambo mengine wametoa msaada wa vitu mbalimbali ikiwemo chakula kwenye kituo cha kituo cha kulelea watoto cha Brother of Charity kilichopo Kata ya Kitangili Manispaa ya Shinyanga

 

Kamati ya utekelezaji jumuiya ya wazazi Wilaya ya Shinyanga mjini  ikitembelea na kukagua ujenzi wa daraja la Kitangili leo Ijumaa Mei 12,2023 ikiwa ni sehemu ya ziara ya kutembelea na kukagua uhai wa jumuiya kwenye kata katika Wilaya hiyo ya Shinyanga mjini.


Share To:

Misalaba

Post A Comment: