📌 Ni katika kuongeza tija ya upatikanaji wa umeme wa kutosha kwenye gridi ya Taifa
📌Asema huu ni muendelezo wa juhudi za Serikali kuhakikisha umeme unapatikana kwa wingi na kuwanufaisha wananchi
📌Akagua mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli na njia ya kusafirisha umeme Ibadakuli-Simiyu
📌Mradi wafikia zaidi ya asilimia 89, Majaribio ya baadhi ya mitambo yaanza rasmi
Naibu Waziri wa Nishati, Mheshimiwa Salome Makamba, amesema mradi wa umemejua unaotekelezwa wilayani kishapu mkoani Shinyanga utaleta mapinduzi makubwa kwenye sekta ya nishati na kiuchumi kutokana na kutoa mchango mkubwa wa upatikanaji wa umeme wa uhakika utakaoingizwa kwenye gridi ya Taifa.
Mhe Salome ameyasema hayo leo tarehe 9 Januari,2026 akiwa mkoani Shinyanga mara baada ya kutembelea mradi wa umemejua wa kishapu pamoja na ule wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli sambamba na njia ya kusafirisha umeme kutoka Ibadakuli-Simiyu.
Amesema huu ni muendelezo wa jitihada za Serikali kupitia Mhe Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kuhakikisha wananchi wananufaika na miradi inayotekelezwa na Serikali hususani ya umeme.
Kuhusu mradi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme cha Ibadakuli na ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme Mhe.Salome amesema umeme utakaozalishwa utawanufaisha wananchi wote wa Tanzania na kuleta mapinduzi kwani sekta ya umeme inawagusa mwananchi mmojammoja.
Akizungumzia maendeleo ya mradi huo, Meneja mradi wa Kishapu Mha.Emanuel Anderson amesema, mpaka sasa mradi umefikia zaidi ya asilimia 89 na unahusisha ujenzi wa paneli elfu 82 zenye uwezo wa Wati 605 kika moja zitakazozalisha megawati 50 za awali kwa awamu ya kwanza
Amesema mradi wa umemejua kishapu utakuwa wa manufaa makubwa kutokana na umuhimu wake kwenye utunzaji wa mazingira unaoepuka uzalishaji wa hewa ya ukaa na umeajiri Watanzania wengi kwa kipindi chote cha utekelezaji wake.
Akitoa tathmini ya ujenzi wa upanuzi wa kituo cha kupoza umeme Kaimu Mkurugenzi wa Miradi ya umeme TANESCO makao Makuu Mha. Frank Mashalo amesema miradi hiyo inahusisha uongezaji na uwekaji wa Transfoma yenye uwezo wa MVA 780 ili kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa Mkoa wa Shinyanga na Mikoa jirani.
Aidha ameeleza kuwa miradi hiyo inatekelezwa na Mkandarasi Sieyuan Electric kutoka China na Kalpataru kutoka India anayetekeleza mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu.
Awali kabla ya kuanza ziara yake Mhe Salome na ujumbe wake walipata fursa ya kumtembelea Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe.Mboni Mhita ambaye alimshukuru Mhe.Salome kwa kazi nzuri anayoifanya kutembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ya nishati chini ya taasisi zake.
Miradi yote ya upanuzi wa kituo cha kupoza umeme njia ya kusafirisha umeme kutoka Shinyanga hadi Simiyu na ule wa umemejua wa kishapu imegharamiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa asilimia mia moja.









Post A Comment: