Waziri wa Nchi Ofisi ya  Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Mhe. George Simbachawene amewataka viongozi wa dini zote nchini kuendelea kuliombea Taifa amani, utulivu  pamoja na kukemea vitendo viovu vya mmomonyoko wa maadili vinavyoendelea duniani kote.

Waziri Simbachawene ameyasema hayo wakati alipomuwakilisha Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa Majaliwa katika Ibada ya Harambee ya uchangishaji fedha katika Usharika wa Kongwa, Dayosisi ya Dodoma ambapo ameahidi kuchangia milioni kumi kwa ajili ya kumalizia jengo la Kanisa hilo huku akimbatana na viongozi mbalimbali wa Mkoa  wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa Rosemary Senyamule na Spika Mstaafu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mbunge wa Jimbo la Kongwa Mhe. Job Ndugai.

"Mhe. Rais amekuwa akitoa wito kila siku ya kwamba mara zote tukumbuke kuiombea nchi yetu iwe na amani, mshikamano, ustawi, mafanikio na maendeleo lakini pia tuliombee Taifa letu ili kuepukana na mmomonyoko wa maadili ambao unaathiri Utamaduni wa Taifa letu niwaombe msiache kuliombea kila mnapofanya ibaada zenu" Amesema Simbachawene

Akitoa salamu za Serikali Simbachawe ametoa rai kwa waumini hao kuiombe nchi amani, upendo, utulivu na mshikamano kwakuwa nakusisitiza kuwa ustawi wake ndio chachu ya maendeleo

Mhe. Simbachawene pia ametumia fursa hiyo kukukemea vikali kuhusu mmonyoko wa maadili, mahusiano ya ndoa za jinsia moja na kuwaasa waumini kusimama katika maagano ya Mungu na kuwaomba maaskofu kuendelea kukemea na kuomba kwakuwa hakuna sababu za kuogopa. 

Simbachawene amesema Serikali inatambua mchango wa Kanisa katika kukuza sekta ya Elimu, Afya na Maendeleo ya jamii kwa kuwa kichocheo kikubwa katika kutukuza neno la mungu kupitia huduma wanazotoa.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amewapongeza waumini wa usharika huo kwa kuendelea na ujenzi wa kanisa hilo ambao ujenzi wake unagharimu zaidi ya Shilingi milioni 360 hadi kukamilika kwake ambapo hadi sasa zaidi ya Shilingi millioni 203  zimekwishatumika.

"Hongereni sana kwa hatua mliyofikia ya ujenzi mmefika sehemu nzuri, mmeangalia Dodoma kama Makao Makuu ya Nchi na nyie mmejenga Kanisa la kimakao Makuu kweli kweli niwapongeze sana na Mungu awabariki" amesema Mhe. Senyamule 

Naye Askofu wa Kanisa la KKKT Dayosisi ya Dodoma Christian Ndossa amesema Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeendelea kuonyesha ushirikiano kwa madhehebu mbalimbali huku akiwataka watanzania kuacha uvivu wa kusoma na kusikiliza neno la Mungu na kukimbilia  miujiza  isiyo na kweli ndani yake. 

Askofu huyo amesema shina la uharibifu limesimama hivyo wanadamu wamepotea kwa kukosa maarifa, na kutoa rai kwa waumini kurarua mioyo yao na si mavazi.

"Tusimame katika nafasi zetu kwa kusimamia maandiko matakatifu na kuendelea kumuomba Roho Mtakatifu kusaidia katika kufanikisha mambo ambayo kwa macho ya kibinadamu yanaonekana hayawezekani" Amesisitiza Askofu Ndossa

Takriban kiasi cha shilingi Milioni 77.8 kimepatikana kupitia harambee hiyo na mifuko 270 ya saruji kwa lengo la kukamilisha ujenzi wa jengo hilo la kanisa la KKKT Dayosisi ya Kongwa.

Share To:

Post A Comment: