Serikali  imesema itaendelea kutoa miradi mbalimbali ya ujirani mwema kwa jamii zinazoishi pembezoni mwa maeneo ya Hifadhi hasa kwenye vijiji ambavyo vitaongoza kudhibiti matukio ya ujangili wa wanyamapori.

Kauli hiyo imetolewa leo Mei 7, 2023 na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Mary Masanja (Mb) katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye kijiji cha Bisarara Wilayani Serengeti Mkoani Mara ikiwa ni mwendelezo wa ziara ya Mawaziri Watatu kutoka Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na Wizara ya Maliasili na Utalii ya kusikiliza kero za wananchi.

“Kuhusu suala la miradi ya ujirani mwema, kuna baadhi ya maeneo bado ujangili unaendelea na utaratibu uliopo hivi sasa ni kwamba tutapeleka miradi hiyo kwa kijiji ambacho kimepunguza au kumaliza kabisa matukio ya ujangili” Mhe. Masanja amesisitiza.

Amefafanua kuwa Serikali iliweka utaratibu wa kutoa miradi hiyo kwa wananchi waishio pembezoni mwa hifadhi ili kuwawezesha wananchi hao kujikwamua kiuchumi.

Mhe. Masanja amewataka wananchi kufuata sheria za nchi, kutii sheria bila shurti, kuacha uwindaji na ujangili wa wanyamapori ili kuendana na matakwa ya Serikali ya kulinda rasilimali za Taifa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na vijavyo.

Aidha, kuhusu ombi la wananchi la kujengewa uzio ili kuzuia wanyama wakali na waharibifu hususan tembo kuvamia makazi ya watu, Mhe. Masanja amesema Serikali imepokea ombi hilo na iko kwenye mchakato wa kulifanyia kazi.

Ameweka bayana kuwa Serikali inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan inawapenda sana wananchi na ndio maana imetuma ujumbe wa Mawaziri watatu kusikiliza changamoto za wananchi.

Katika hatua nyingine, Mhe. Masanja amewaasa wananchi hao kuacha tabia ya kuingiza mifugo hifadhini kwani haina tija kwa Taifa

“Wafugaji wote nchi nzima sehemu ya kuchungia si maeneo ya Hifadhi kwenye Hifadhi kuna sheria zake hivyo  tuziheshimu” Mhe. Masanja amesema.

Share To:

Post A Comment: