Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Senyamule amemuagiza Mkuu wa Wilaya Chemba kusimamia kwa karibu ukamilishaji wa ujenzi wa madarasa katika Wilaya yake ndani ya muda uliopangwa.

Senyamule ametoa agizo hilo leo tarehe 27 Mei, 2023 baada ya kufanya ziara ya kikazi katika Wilaya ya Chemba na Kondoa kukagua ujenzi wa madarasa kupitia fedha za boost.

Akiwa Wilayani Chemba katika Shule ya Msingi Soya Senyamule ameonyesha kutoridhishwa na maendeleo ya ujenzi katika Shule hiyo na kuhoji endapo wanajua ni lini madarasa hayo yanatakiwa kukamilika.

"Sijafurahishwa kabisa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule hii, tunapotoa maelekezo ni lazima yazingatiwe. Tarehe 20 Juni 2023 kazi inatakiwa kukamilika, Wilaya ikabidhi kwa Mkoa tupate muda wa kufanya ukaguzi ili nasi tarehe 30 Juni 2023, tukabidhi TAMISEMI" Senyamule alisisitiza.

Senyamule amesema nia na dhamira ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni kuhakikisha miradi hususan ya ujenzi wa Shule na Vyumba vya madarasa unakamilika kwa wakati, hivyo ni vema kila mtendaji kuhakikisha anaenda sawia na spidi ya Mheshimiwa Rais.

Akiwa Wilayani Kondoa Senyamule amekagua pia ujenzi wa Shule mpya ya msingi yenye madarasa 7 na madarasa 2 ya awali katika eneo la ‘Maji ya Shamba’ na Shule ya Msingi Miningani ambapo ujenzi wa madarasa 6 unaendelea.

"Nahitaji kupewa taarifa ya kila siku ya mwenendo wa ujenzi wa Shule hizi na madarasa yake. Tunaposema kukamilika, tukabidhiwe darasa na madawati yake ndani" Senyamule alifafanua.

Mkuu wa Wilaya ya Chemba Mhe. Gerald Mongella na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Kondoa Bw. Paul Sweya wamemhakikiashia Mkuu wa Mkoa kuwa watahakikisha usimamizi madhubuti wa ujenzi na Shule na madarasa ili yaweze kukamilika kwa mujibu wa mpango kazi.

Mkoa wa Dodoma kupitia mradi wa Boost umepokea kiasi cha Shilingi Bilioni 10.6 kwa ajili ujenzi wa Shule mpya 16, vyumba vya madasa ya msingi 163, madarasa ya awali 16, ujenzi wa vyoo 106, nyumba za walimu 03 na darasa 01 la elimu maalumu. Wilaya ya Chemba imepokea kiasi cha shilingi Bilioni 1.3 na Kondoa Mji na Halmashauri Shilingi Bilioni 1.7
Share To:

Post A Comment: