Na Imma Msumba ; Karatu

HARUFU ya ufisadi imejitokeza katika ujenzi wa soko la wafanyabishara  wadogo la Karatu, ikielezwa limejengwa chini ya kiwango.

Hayo yameibuliwa na uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Arusha, kupitia mwenyekiti wake, Zelothe Steven.

Uongozi wa CCM Mkoa umeonyesha kutoridhishwa na mradi wa soko hilo linalojulikana kama Soko la Machinga la Karatu kwa maelezo kwamba umejengwa chini ya kiwango.

Katika maekezo yake, Mwenyekiti Zelothe amesema CCM imekataa kupokea mradi wa soko la machinga na kumwagiza Mkuu wa Wilaya ya Karatu, Dadi Kolimba, kuwachukulia hatua mara moja watumishi wote wa halmashauri waliohusika kuhujumu ujenzi wa soko hilo.

Aidha Chama cha Mapinduzi kimekerwa na ujenzi wa choo kilichogharimu milioni 15 katika soko hilo ambacho thamani ya fedha haiendani na choo hicho cha soko hilo.

Kufuatia hali hiyo, Zelothe akizungumza Kwa niaba ya wajumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Arusha alisema; 

"MKuu wa wilaya hapa hakuna soko la machinga haiwezekani shilingi milioni 12 zitumike kujenga Soko hili ambalo thamani ya fedha haiendani na thamani ya fedha iliyotumika hususani na kwenye Choo.Wote waliohusika akiwemo Mhandisi wa ujenzi wa halmashauri wachukuliwe hatua mara Moja".

Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Karatu Daniel Awack amesema ameeomba mchoro wa soko hilo ili aweze kutoa fedha kiasi cha shilingi milioni nane lakini mpaka sasa ni zaidi ya wiki tatu hajapewa huo mchoro.

Alisema zimebaki siku thelathini mwaka wa fedha wa serikali umalizike na kwamba ana hofu fedha hizo ambazo ni za mfuko wa jimbo kurudishwa kutokana na kukosekana kwa mchoro ambao uongozi wa Halmashauri ya Mji mdogo wa Karatu iliupitisha.

Mwenyekiti wa Mamlaka ya Mji mdogo wa Karatu Yuda Morata alisema waliridhia kwenye kikao kuwa lijengwe soko lenye nguzo za chuma lakini badala yake wameweka nguzo za mbao.

Alisema choo kilijengwa kwa kutumia baadhi ya vifaa vilivyobaki kwenye nyumba za watumishi ambao ni wakuu wa idara.

"Ramani iliyojengwa hapa kwenye hili soko siyo ramani tuliyokubaliana Nina mashaka pia kama kuna ramani ya soko kwa sababu tulichokubaliana kwenye kikao sicho kilichojengwa lakini pia fedha zilizotumika kwenye ujenzi wa soko hili ni nyingi ikilinganishwa na kazi iliyofanyika hapa," alisema.

Ramadhan Juma Katibu wa CCM kata ya Karatu alisema mradi huo umekuwa ukifanywa kwa usiri mkubwa ambapo uongozi wa machinga,viongozi wa kata hiyo hawakushirikishwa juu ya mradi huo na wanapohoji hawapati majibu kutoka kwa Mhandisi huyo.

"Machinga wanapata tabu wanazunguka mjini wakati serikali imetenga fedha za kuwajengea soko na sisi viongozi tunaulizwa na machinga kila siku ni lini soko litakamilika lakini hakuna majibu.

"Hata sisi viongozi hatujashirikishwa kwenye huu mradi wala viongozi hali inayosababisha tunakosa majibu ya kuwapaachinga na wananchi wengine wa kawaida wanaohitaji kupata huduma za machinga," alisema.



Share To:

Post A Comment: