Wafugaji kote nchini katika msimu huu wa mvua  wametakiwa kutenga baadhi ya maeneo ya malisho na kuyahifadhi kwa ajili ya matumizi wakati wa kiangazi  ili kuepuka migogoro baina yao na wakulima.

Kamanda wa Kikosi cha Kuzuia wizi wa Mifugo Nchini ACP Simon Pasua ameyasema hayo leo wilayani Monduli wakati alipokutana na viongozi wa wafugaji pamoja na wakulima kwa lengo la kupanga mikakati ya pamoja ya kuepusha migogoro ambayo imekua ikijitokeza wakati wa kiangazi.

Kamanda Pasua amebainisha kuwa wakati wa kiangazi kuna kuwa na ukame hivyo kupelekea changamoto za kukosekana sehemu za malisho hali ambayo inasababisha baadhi ya wafugaji kupeleka mifugo sehemu ambazo sio rasmi.

Lakini pia amewataka kupanga matumizi bora ya ardhi pamoja na kuacha kupelekea mifugo maeneo ya vyanzo vya maji ili kuepuka migogoro ambayo inaweza kujitokeza lakini pia kukauka kwa vyanzo hivyo.

Mwisho ametoa wito kwa wafugaji pamoja na wakulima kuwa na vikao vya maridhiano na kutumia vikundi vya ulinzi shirikishi pindi migogoro inapotokea kuepuka uvunjifu wa amani. 

Kwa upande wake Bwana Julius Mariki ambaye ni kiongozi wa Wafugaji Kijiji cha Mungere pamoja na kushukuru ujio wa mkuu huyo amesema ushirikiano ni suala la muhimu hivyo akaomba kuwepo na vikao ambavyo vitawakutanisha wadau mbalimbali wa mifugo pamoja na kilimo ili kuondoa tatizo la migogoro.

Naye bwana Anthony Mroso ambaye ni mkulima mkazi wa Kijiji cha Majengo wilayani Monduli ameiomba serikali kuweka mipaka katika kijiji hicho ambayo itaonesha maeneo ya kilimo, makazi pamoja na ya malisho.


Share To:

mwangaza wa hbari

Post A Comment: