Na,Imma Msumba ; Arumeru 

Ukame na majanga mengine yanayohusiana na maji yanaongezeka kwa kasi kubwa sana nchini Tanzania kutokana na mabadiliko ya tabianchi na, ukizingatia ongezeko la idadi ya watu duniani na kupungua kwa upatikanaji wa rasilimali hiyo katika maeneo mengi huku idadi ya watu wanaoathirika na matukio haya inaongezeka.

Mabadiliko ya Tabia Nchi yamesababisha mabadiliko ya mvua kimataifa na kikanda kwa sababu ya ongezeko la joto duniani yanabadilisha mwelekeo wa mvua na msimu wa kilimo, na kuathiri uhakika wa chakula na ustawi wa binadamu.

Jumla ya maji yote ya juu ya uso wa dunia na katika chini ya ardhi, ambayo ni pamoja na barafu, yamepungua kwa sentimita moja kila mwaka katika kipindi cha miaka ishirini iliyopita huku hali ikizidi kuwa mbaya kwani asilimia 0.5% ya maji hayo ndiyo yanaweza kutumika kama maji safi na salama kwa ajili ya matumizi ya binadamu.

Ili kufanikisha ustawi wa muda mrefu wa kijamii, uchumi na mazingira duniani kunahitajika usimamizi jumuishi wa rasilimali za maji.Lakini nchi 107 duniani kote haziko kwenye njia sahihi kufikia lengo la kusimamia rasilimali zao za maji endelevu ifikapo 2030.

Nchini Tanzania lengo kuu la Serikali ni kuendeleza huduma za maji kuanzia miaka ya 1970, kiwango cha upatikanaji wa huduma hizo sio cha kuridhisha. Lengo la Sera ya Maji ya 1991 lilikuwa kuwapatia wananchi wote maji safi na salama katika umbali usiozidi mita 400 ifikapo mwaka 2002. Utekelezaji wa lengo hili unaonesha kuwa karibu 50% ya wananchi walio vijijini ndio wanaopata huduma hiyo. Kiwango halisi ni chini ya hapo, kwani zaidi ya 30% ya miradi iliyojengwa vijijini haifanyi kazi vizuri kutokana na hali duni ya matengenezo na uendeshaji.

Hapa Tanzania, kiasi cha maji yanayofaa kwa matumizi ya binadamu na kinachopatikana kwa sasa ni kilomita za ujazo 89 sawa na mita za ujazo 2,700 kwa mtu kwa mwaka. Kufuatia ongezeko la watu nchini kutoka milioni 33 mwaka 2001, hadi milioni 59.8 ifikapo mwaka 2025, kiasi hiki cha upatikanaji wa maji kwa mtu kwa mwaka kitapungua kwa 45% na kufikia mita za ujazo 1,500, ikiashiria kwamba wakati huo patakuwepo na uhaba wa maji, kwani kiasi cha maji chini ya mita za ujazo 1,700 kwa mtu kwa mwaka ni kiwango kinachoonesha kuwa kuna uhaba wa maji.

Kata ya Mwandet yenye vijiji {4} na vitongoji {14} iliyopo Wilayani Arumeru Mkoani Arusha ambapo wananchi wanakabiliwa na huduma ya maji safi na salama ambapo wanawake,wanafunzi na wasichana ndio wahanga wakubwa wa changamoto hii ambapo hutembea umbali mrefu kutafuta maji ambayo huyatumia kwa shughuli za matumizi ya majumbani na mashuleni.

Shule na Kituo vya Afya ambavyo ndio vituo vinavyotoa huduma muhimu za Afya na Elimu katika Kata hiyo havina huduma za msingi za maji safi na salama jambo linalowafanya wananchi wanaoishi katika eneo hilo kuendelea kuteseka kupata huduma hizo muhimu ingali majengo yapo,ikumbukwe Tanzania ipo katika hatari kubwa ya mabadiliko ya Tabia ya nchi ambapo joto limeongezeka, na ukame ni wa mara kwa mara ambapo mabwawa na visima vya kuhifadhia maji vinakauka ambapo watu wanaoishi katika jamii za kipato cha chini/duni ndio waathirika zaidi wa huduma ya maji safi na salama.

Logolie Masandawa Lukumay ni Diwani wa Kata ya Mwandet katika Halmashauri ya Arumeru anaeleza kuwa mabadiliko ya Tabia nchi yamewaadhiri kwa aslimia zaidi ya 90% kwani wananchi wa kata yake wanalazimika kuamka alfajiri na kutembea mchana kutwa kwenda kutafuta maji kwa zaidi ya kilomita {35} na hata muda mwingine wananchi hao kurudi bila ya kupata huduma ya maji safi na salama.

“Wananchi wanaenda kufuata maji mpaka kwenye Kata ya Lengijave na Olkokola ambapo ni umbali mkubwa sana kwani wanantoka asubuhi sa kumi na mbili asubuhi na kurejea jioni saa kumi siku nzima wanaitumia kwenda kutafuta maji na kuacha shughuli za kuwaingizia kipato na za kuendelea kulijenga Taifa”

“Kwa upande wa pili kule Kata yetu imepakana na Wilaya ya Monduli na kule kuna mfereji unaotiririsha maji mengi sana ila ni kwa muda mfupi sio wakuutegemea sana kwani muda mwingine nao unakuwa hautiririshi maji ikitokea wakienda wakikosa maji inawalazimu kurudi kuja kujipanga upya kwa ajili ya kesho yake kwenda kwenye maeneo mengine ya Kata za jirani” Aliongezea

“Kata nzima hii inachangamoto sana na huduma ya maji safi na salama ila hapa tulipo ni Kijiji cha Engalaoni,Watoto wengi wa Kijiji hiki wanaenda shuleni mara chache sana muda mwingi wanautumia kujumuika na wazazi wao kwenda kutafuta maji na kupeleka mifugo kupata maji” Alisema

“Mimi kama kiongozi naogopa kupita katika maeneo ambayo wananchi wanapata pata maji kwa muda huo kwani wananchi wanaweza kuwa na changamoto nyingine wakatamani hata kukudhuru kutokana na ugumu wa maisha wanaopitia na mambo mengine ambayo sio mazuri”

“Watoto wanalazimika kutoka na maji majumbani hata kwenye kidimu cha lita tatu ila kwa upande wa kile Kituo cha Afya Engalaoni Serikali isipojitahidi kuleta maji hapa kwa haraka pale hapatakuwa na kitu chochote kitakachoendelea hususani katika utoaji wa huduma za Afya itakuwa ni bure tu” Alisema Lukumay

Lakini Pia niishukuru Serikali kwani inaendelea kujitahidi kwa kweli kwa sasa imeweka mkakati mzuri kwa kutuletea mradi wa maji ambao unatokea katika mnada wa Losikito na maji mengine yale yaliyozinduliwa na Marehemu Rais John Pombe Magufuli kutoka kwenye mradi wa Bilioni 520 ambao wananchi wataunganishwa nao kutoka Kata ya Lengijave,Serikali iiende spidi katika kutekeleza mradi huu ili wananchi waweze kufikiwa na huduma hii ya maji ili kupunguza adha hii na sio vinginevyo.

Kwa upande wake Meneja wa Usambazaji wa Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Arumeru Mhandisi Sabiri Waziri amesema mwazoni wa mwezi wa pili mwaka huu mkandarasi amepatikana na kukabidhiwa eneo la ujenzi (site) mwezi wa tatu ambapo amepewa mkataba wa mwaka mwaka kuhakikisha Kijiji cha Engalaoni huduma ya maji inawafikia na kusambaza katika maeneo mengine matano (5) yanayozunguka Kijiji hicho.

“Mkandarasi yupo eneo la ujenzi na ameshaanza kazi na kwa sasa anaendelea kumwaga malighali (material) ka ajili ya ujenzi wa tanki na malighafi mengine kwa ajili ya vituo vitano vya kusambazia maji” Alisema Menenja

“Serikali tumeshasikia kilio cha wananchi wa Kijiji cha Engaloni waendelee kuwa na Subira kwani tatizo la maji katika Kijiji chao litatatuliwa ndani ya mwaka mmoja kwani tayari mradi umeanza kutekelezwa na unagharimu Milioni 595,826,353.50 kutoka mfuko wa maji, ila kwa sasa waendelee kupata maji hivyohivyo kupitia ule mtandao wao wa zamani ingawa kipindi cha kiangazi ulikuwa sana na shida ila natumaini hivi sasa mvua za siku mbili hizi wataendelea kuchota maji ili mradi huu utakapokamilika wataweza kupata maji muda wote kipindi cha kiangazi na masika kwa kupitia mradi huu mpya” Alisema




Share To:

Post A Comment: