Na, Imma Msumba; Moshono

Afya ya mama na mtoto ni mfumo wa utoaji huduma maalum kwa wanawake walio katika umri wa uzazi na watoto wenye umri chini ya miaka mitano, hasa watoto wachanga tangu kuzaliwa hadi siku 28. Huduma hizi zinajumuisha kutambua vidokezo hatari kwa wanawake na watoto, chanjo, tiba, elimu ya uzazi, uzazi salama, mbinu shirikishi za udhibiti wa magonjwa ya watoto, afya katika jamii, lishe na afya shuleni.

Dunia imepiga hatua kubwa katika kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga katika miongo ya hivi karibuni. Vifo vitokanavyo na uzazi vimepungua kwa karibu asilimia 40 tangu mwaka 2000, na vifo vya watoto wachanga vimepungua kwa karibu asilimia 50 tangu mwaka 1990.

Vifo vingi vya akina mama na watoto wachanga leo vimejikita katika mazingira dhaifu na miongoni mwa wanawake na watoto wachanga walio katika mazingira magumu ambao wanakabiliwa na vikwazo vya kupata huduma bora na za kuokoa maisha. Kifo cha mwanamke wakati wa ujauzito au kujifungua kinatishia uwezekano wa mtoto wake kuishi, hupunguza nafasi za watoto wake wengine kuishi na elimu, na kutishia utulivu wa familia yake. Hatimaye, vifo vya akina mama na watoto wachanga vinadhoofisha ustawi wa nchi.

Juhudi kubwa zimefanyika na Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na wananchi na wadau mbalimbali katika kupanua, kuboresha na kusambaza huduma hizo kwa walengwa. Aidha, huduma za chanjo na mnyororo baridi zimeonyesha mafanikio makubwa na kuifanya nchi yetu kupata medali ya kimataifa na kuwa mfano wa kuigwa katika bara la Afrika. Hata hivyo, pamoja na mafanikio hayo, bado vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga vimeendelea kuwa juu. Kiwango cha vifo vya wanawake kimeongezeka kutoka 529 mwaka 1996 hadi kufikia 578 mwaka 2005 kwa kila watoto 100,000 waliozaliwa hai. Kutokana na hali hiyo upo umuhimu wa kuongeza juhudi katika utoaji wa huduma hii ili kupunguza vifo vya wanawake wajawazito na watoto wachanga kwa kiasi kikubwa.

Serikali nchini Tanzania imeendelea kupambana kwa kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo na athari za magonjwa kwa wanawake wajawazito, pamoja na watoto wenye umri chini ya miaka mitano hasa watoto wenye umri chini ya mwaka mmoja kulingana na Malengo ya Milenia.

Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inayotoa huduma bila faida, na mashirika ya kimataifa, itaendelea kutoa huduma bila malipo kwa; wanawake wajawazito, watumiaji wa huduma za uzazi wa mpango na watoto wenye umri chini ya miaka mitano,Pia kuendelea kuaandaa na kusimamia utekelezaji wa miongozo, mikakati na mipango endelevu ya kupunguza vifo vya wanawake vinavyotokana na uzazi pamoja na vifo vya watoto wenye umri chini ya miaka mitano hasa watoto wachanga kwa kuwapatia huduma za dharura. Kushirikiana na wadau mbalimbali na wananchi kuboresha miundo mbinu ili kuwawezesha; wanawake wajawazito na watoto wachanga kufikiwa na kutumia huduma za afya. Kuendelea kuhamasisha na kuelimisha wananchi hasa wanawake kuhusu umuhimu wa huduma za afya.

Hususani kuelewa kwamba wanawake wengi hawawezi kufikia vituo vya afya mara kwa mara na wanaweza kukosa fursa za huduma za kinga na tiba, pia tunashirikiana na kuimarisha ubora na ufikiaji wa huduma za afya ya jamii vijijini na mijini.

Isaya Doitha ni Diwani wa Kata ya Ngarenaro ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Afya,Elimu na Uchumi katika Halmashauri ya Jiji Arusha anaeleza kuwa wananchi wa Kijiji cha Olkeryan kwa muda mrefu wamekuwa wakikosa huduma za afya kutokana na kutokukamilika kwa jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Jengo la Mama na Mtoto (RCH) ambayo imekuwa ni changamoto ya muda mrefu katika eneo hilo.

“Majengo yapo katika hatua ya ukamilishaji ambapo tunatarajia mwezi julai majengo yale yataanza kufanya kazi na kutoka huduma kwa wananchi kama ilivyokusudiwa,kila kitu kipo katika hatua za mwisho kinachohitajika kwa sasa ni Mkurugenzi wa Jiji sasa kupeleka wataalamu ili wananchi wetu wa Kata ile ya Moshono waweze kuondokana na adha ya kutembea umbali mrefu kufuata huduma za matibabu” Alisema Doitha

“Kwa kweli katika eneo lile huduma zipo mbali na Kata ile ni kubwa sana na wanachi wanatembea umbali mrefu kwenda kutafuta huduma ya matibabu maana jiografia ya usafiri na mabasi katika eneo lile nayo ni ngumu sana ila tunapambana kukamilisha Kituo kile ili wananchi wapate huduma waone sisi kama serikali tumewasogezea huduma maana ndiyo kazi yetu kupeleka huduma kwa wananchi wenye uhitaji”Aliongezea

“Ni kweli zimetumika Zaidi ya milioni 100 kwa ajili ya ujenzi lakini kwa sasa mkandarasi yupo kazini na anamalizia kuweka madirisha,marumaru (Tiles) Pamoja na milango” Doitha aliongeza.

Kwa Upande wake Diwani wa Kata ya Moshono Bi. Miriam Kisawike ameeleza kuwa kucheleweshwa kwa huduma ya Afya kwa wananchi wa Olkeryan ni changamoto kubwa sana kwani mategemeo ya wananchi yalikuwa ni kupata huduma lakini kutokukamilika kwa majengo hayo wananchi wameendelea kuteseka.

“Mimi kama Diwani niiombe tu Serikali sambamba na Halmashauri ya Jiji kufanya jitihada za haraka ili majengo yale yaweze kukamilika haraka na wananchi waanze kupata huduma” Alisema Bi. Miriam

“Kituo kilichopo ambacho ni cha zamani ni Zahanati wananchi pale wanapata huduma mpaka saa tisa mchana,matarajio yetu kukamilika kwa majengo yale huduma za Afya zingeongezeka na kutolewa mpaka usiku maana wananchi wangu bado wanatembea umbali mrefu kwenda kupata huduma hususani kwa kina mama wajawazito na Watoto wadogo pindi wanapoumwa mida ya jioni inawawia vigumusana Kwenda kutafuta huduma katika vituo vilivyo mbali” Aliongezea Mariam

Miriam anaendelea kueleza kuwa kutokukamilika kwa majengo yale kumesababishwa na mafungu ya fedha kuchelewa ambapo anasema hawezi kusema kwamba ni uzembe kwani bajeti ya jingo ilitengwa shilingi Milioni 125 ila zilitolewa milioni 100 mpaka sasa ambapo ndio chanzo kikubwa kilichosababisha mpaka sasa jingo lile kushindwa kukamilika kwa wakati na wananchi wakiendelea kuteseka kusaka huduma za matibabu nyakati za usiku.

“Ila kwa tarifa nilizo nazo mpaka sasa Halmashauri imeongeza shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kukamilisha majengo maana lipo katika hatua za mwisho kabisa ili liweze kukamilika nakuaanza kutoa huduma kwa wananchi wetu wa Kijiji cha Olkeryan na wakazi wamaeneo ya Jirani”

“Nipende kuishauri Serikali kwamba pindi wanapoamua kuanzia mradi ama kama mradi umeanzishwa na wananchi mradi ule usichukue muda mrefu Kwenda kukamilika kwani mradi unapochukua muda mrefu unakumbana na changamoto za mfumuko wa bei ya vifaa ambao ndio sababu kubwa iliyokikumba Kituo cha Afya cha Olkeryan,niwape pole tu wananchi wangu kwa changamoto walizozipitia na wanazoendelea kuzipitia kwani haikuwa mategemeo yetu kwani Kituo kilianza kujengwa tangu mwaka juzi 2021 na tulitegemea ndani ya mwaka mmoja wananchi wangeanza kupata huduma niwaombe wananchi waendelee kuwa tu wavumilivu”Share To:

Post A Comment: