Mgombea ubunge wa Jimbo la Ngorongoro kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Yanick Ndoinyo, ameweka wazi msimamo wake kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ndiye kiongozi wa kwanza tangu uhuru kuwasikiliza viongozi wa kimila wa Ngorongoro na kujadiliana nao changamoto za uhifadhi na ardhi.
“Rais Samia ndiye Rais wa kwanza toka Tanzania ipate uhuru kuwasikiliza viongozi wa kimila zaidi ya 150. Hii imetupa faraja kubwa, ni mama msikivu na tayari kututatulia changamoto. Nawaombeni tumchague awe Rais wetu,” alisema Ndoinyo.
Kauli hiyo aliitoa wakati wa mikutano ya kampeni katika kata za Olbalbal na Ngoile, akisisitiza kuwa wananchi wa Ngorongoro wanapaswa kuendelea kuiamini CCM kwa kazi kubwa zinazotekelezwa na serikali ya awamu ya sita.
Wakazi wa kata za tarafa ya Ngorongoro Nanyai Sungare, mkazi wa Olbalbal na Elius Ngorisa,mkazi wa Ngoile pia walieleza imani yao kwa Rais Samia na wagombea wa CCM.
“Tunamwamini Mama Samia na wagombea wa CCM kwa sababu wamesikiliza kilio chetu.”Alisema Sungare
“Hii ni mara ya kwanza tunaona Rais anashirikiana na viongozi wetu wa kimila. Tunachagua CCM kwa maendeleo.”Alisema Ngorisa
Wilaya ya Ngorongoro, yenye kata 28, inatarajia kuwa na wapiga kura zaidi ya laki moja na sabini kwenye uchaguzi huu, ambapo wananchi wengi wameonyesha dhamira ya kuiunga mkono CCM kuanzia ngazi ya rais, mbunge hadi madiwani.







Post A Comment: