“Huwa naamka mapema sana alfajiri na napeleka mifugo kunywesha maji kisha naelekea malishoni umbali mrefu wa zaidi ya kilomita sita (6) mpaka tisa (9) ambapo huwa tunakaa malishoni mpaka jioni ndipo tunarejea, kipindi cha masika huwa tunawahisha mifugo malishoni alafu mchana ndio tunazileta kunywesha maji”

Haya yalikuwa ni majibu ya Mwagwere Ngorob, Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Engikaret Wilayani Longido alipofanya mazungumzo na mwandishi wetu.

Inasikitisha, inaghadhabisha na kutafakarisha. Lakini je? Tumefikaje hapa?

Jopo la Kimataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (IPCC) lilibuniwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) na Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa (UNEP) ili kuwa chanzo kisichokuwa na upendeleo cha habari ya kisayansi kuhusu mabadiliko ya tabiachi. Katika mwaka wa 2013, IPCC ilitoa ripoti iliyopitiwa na wenzao ulimwenguni kote kuhusu nafasi ya shughuli za binadamu kwa mabadiliko ya tabianchi wakati ilipotoa Ripoti yake ya Tano ya Tathmini. 

Ripoti hiyo ilieleza wazi kwenye hitimisho lake: mabadiliko ya tabia nchi yapo na shughuli za binadamu, haswa kuachiliwa kwa gesi chafuzi kutokana na kuchoma fueli ya visukuku (makaa ya mawe, mafuta, gesi), ndicho chanzo kikuu.

Tanzania ni ni mojawapo mwa nchi Duniani zinazokabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi. Njia moja ya kukabiliana na hali hii ni kuboresha ardhi iliyoharibika.

Uboreshaji wa mandhari- ukifanya vizuri kwa ushirikiano na jamii za kiasili, serikali na wanasayansi- una manufaa mengi kwa mazingira, ukabilianaji wa tabianchi na ya kiuchumi. Pia huchangia zaidi katika nyingi ya Malengo ya Maendeleo Endelevu.

Kwa Tanzania, Serikali imefanya jitihada kubwa za kupambana na mabadiliko ya tabia nchi kwa kuandaa Sera ya Taifa ya Mazingira ya mwaka 2021, Mpango mkakati wa Kitaifa wa kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi 2021, Mpango kabambe wa Taifa wa Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (2022 – 2023) na Miongozo na Kanuni za Biashara ya Kaboni, ikiwa ni jitihada za kukabiliana na mabadiliko ya Tabianchi. 

https://www.msumbanews.co.tz/2022/10/dola-bil192-kutekeleza-mpango-wa-

taifa.html?m=0


Halmashauri ya Wilaya ya Longido ni mojawapo ya Wilaya saba (7) zilizopo Mkoa wa Arusha ambapo nyingine ni Halamashauri ya Wilaya ya Arusha, Karatu, Arumeru,Meru, Monduli na Ngorongoro. Wilaya ya Longido ina eneo la Kilomita za Mraba 7782 ambayo ni sawa na  ya eneo lote la Mkoa wa Arusha.Kwa mujibu wa Sensa ya watu na Makazi ya Mwaka 2022 Wilaya ya Longido ina jumla ya wakazi 123,153  kwa Sensa ya 2022 ambapo wanawake ni 62,954 na wanaume ni 60,199 Makabila makubwa  ni Wamasai kwa asilimia 90.Halmashauri ya Wilaya ya Longido hadi kufikia Mwezi June 2017 ilikuwa na jumla ya watumishi 1,117.Wilaya ina jimbo moja la Uchaguzi, Tarafa Nne (4), Kata Kumi na Nane (18),Vijiji arobaini na tisa (49) na Vitongoji  Mia moja na sabini na tano (175). Halmashauri ina shule za Msingi 54 na Sekondari 9.

Licha ya jitihada hizo za Serikali hali ni tofauti kwa Wilaya ya Longido iliopo  Mkoani Arusha ambapo wananchi wa wilaya hiyo asilimia kubwa ni wafugaji ambao wanakabiliwa na adha kubwa ya ukame uliosababishwa na mabadiliko ya Tabia nchi ambayo yanaathiri nyanda za malisho pamoja na malambo ya kunyweshea mifugo maji.

Mwagwere Ngorob ni Mwanafunzi wa darasa la sita katika shule ya Msingi Engikaret Wilayani Longido ndoto yake atakapomaliza shule hapo baadae ni kuwa mwanajeshi wa kulijenga taifa ila ndoto yake iko mbioni kutokukamiliakutokana na muda mwingi kuutumia katika shughuli za kutafutia malisho mifugo ya familia yao.

“Huwa naamka mapema sana alfajiri na napeleka mifugo kunywesha maji kisha naelekea malishoni umbali mrefu wa zaidi ya kilomita sita (6) mpaka tisa (9) ambapo huwa tunakaa malishoni mpaka jioni ndipo tunarejea,kipindi cha masika huwa tunawahisha mifugo malishoni alafu mchana ndio tunazileta kunywesha maji”Alisema

“Familia yetu tupo sita lakini tunaosoma ni watatu hivyo tunapokezana kupeleka mifugo malishoni,nikirudi kutoka shule nakwenda malishoni kumpokea ndugu yangu ili aweze kurejea nyumbani kuja kupata chakula ama kupumzika,hivyo sina muda mwingi wa kujisomea jioni kwani huwa nachoka sana na pia muda mwingine usiku hurudi malishoni kutafuta mifugo iliyopotea”

“Kuanzia mwaka jana mwezi wat isa (9) na miezi hii miwili iliyopita nilienda shule kwa kusuasua sana kutokana na hali ya ukame ambapo malisho yalikuwa mbali hivyo kutulazimu kwenda kutafuta malisho umbali mrefu na ilitubidi tuwe tunaenda wote kutokana na wingi wa mifugo yetu na usalama wa mchungaji dhidi ya wanyama hatari” Aliongezea

“Serikali itoe elimu kwa wazazi kuhusu umuhimu wa mtoto kupumzika napotoka mashuleni sambamba na kujenga shule za kulala kuzunguka jamii ya kimaasai ili kuweza kusaidia wanafunzi kupata muda mwingi wa kujisomea na kukaa shuleni kuliko kutuacha kurudi nyumbani jambo linalotufanya kukosa muda wa kupumzika na kujisomea wakati wa jioni na tuwepo majumbani” Alisema

Kwa Upande wake Afisa Ustawi wa Jamii Longido Bi. Atuganile Chisunga ameelezea kuwa mabadiliko ya tabia nchi yameweza kuwaadhiri kwa kiasi kikubwa sana wilayani humo hususani jamii ya kifugaji na wao kama Serikali wameendelea kutoa elimu kupitia vikao vya vijiji na kuwashauri Wazazi kuwapeleka Watoto mashuleni na sio Kwenda kutafutia mifugo malisho.

“Serikali kupitia Waratibu Kata wa Elimu wamekuwa wakiwachukulia hatua mbalimbali za kinidhamu wananchi wote ambao wamekuwa wakikaidi maelekezo ya Serikali ya kuwapeleka watoto shule” Alisema

“Sisi kama Ustawi wa jamii tutaendelea kutoa elimu katika maeneo yote ya Longido juu ya umuhimu wa Elimu kwa mtoto kwa kuwasihi wazazi kuwapeleka Watoto shule mara umri wa kuwapeleka shule unapofika kwani jamii hii ya kimaasai wanategemea sana ufugaji katika kuendesha maisha yao ya kila siku” Aliongezea

Diwani wa Kata ya Engikaret David Naandi Laizer anaeleza kuwa kwa mwaka 2023 zaidi ya wanafunzi 711 wameandikishwa darasa la awali katika shule mbalimbali kwani Kata yake inajumla ya shule nne za msingi zinazomilikiwa na Serikali huku shule mbili zikimilikiwa na watu binafsi.

“Matokeo kwa mwaka jana hayakuwa mazuri sana kwani Watoto wengi sana walifeli kutokana na changamoto mbalimbali na kushindwa kuendelea na elimu ya sekondari ndio maana unaona vijana wengi wadogo wameamua kujiendeleza kwa kuamua kuwa wafugaji kwa kuchunga mifugo ya wazazi wao” Alisema

“Watoto ni wengi sana katika Kata yetu hii na wanhitaji kupatiwa elimu nilishawasilisha katika baraza ili Halmashauri waangalie namna bora ya kujenga Shule ya Sekondari katika Kata yetu maana kama unavyofahamu jamii yetu ya kimaasai kutoka boma moja hadi jingine ni Zaidi ya kilomita mbili mpaka tatu sasa kwa kata nzima bila kuwa na shule ya sekondari ni changamoto kwa kweli na matatizo kama hayo ya Watoto kwenda kuchunga na kujiajiri bado ni changamoto”

“Tunaishukuru Serikali iliona hili mapema na imetujengea Chuo cha Veta pale Kata ya Orbomba lakini Chuo kile kimkamilika ila tunaiomba serikali sasa ianze kudahili wanafunzi ili Watoto wetu waanze masomo ya ufundi stadi kwani maisha ya sasa yanaenda kisasa haiwezekani kazi za ufundi zinafanywa na watu wa Wilaya nyingine wakati ni fursa kwa vijana wetu wa Wilaya ya Longido” Alisema Diwani

“Kwa sasa ndugu mwandishi nina changamoto sana ya maji katika Kijiji cha kiserian ambayo imekuwa kero sana nalazimika kutoa hela zangu binafsi kuleta maji katika zanahati na shule ili wananchi waweze kupatiwa huduma ,hakuna chanzo chochote cha maji katika Kijiji hicho walikuwa wanategemea bwawa moja bwawa lile limekauka limekuwa tope pundamilia na twiga wanafia kwenye bwawa fisi wanawala kulekule kwahiyo huduma yam aji inakuwa hakuna tena” Amesema




Share To:

Post A Comment: