Katika juhudi za kuboresha miundombinu na kuinua uchumi wa wakazi wa wilaya ya Mbinga, Meneja wa Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wilayani humo, Mhandisi Oscar Musa, amesema mradi wa Agri-Connect unaotekelezwa katika barabara ya Utili–Mahande umefikia hatua muhimu ya ujenzi.
Mradi huo wenye urefu wa kilomita 14.4 na thamani ya shilingi bilioni 16.5 ulianza kutekelezwa mwezi Novemba 2024 na unatarajiwa kukamilika Mei 2026, ikiwa ni kipindi cha miezi 18. Kwa sasa, kazi ya kuchonga na kufungua barabara yote imekamilika, huku ujenzi wa madaraja saba ukiendelea sambamba na uwekaji wa tabaka la udongo ambapo kilomita 8 tayari zimekamilika.
Mhandisi Musa amesema kwamba mradi huo unatekelezwa na Mkandarasi kutoka kampuni ya Ovans Construction Ltd iliyoko Mbinga.
“Lengo kuu la mradi huu ni kuwahudumia wananchi wa vijiji vya Utili, Mahande na Mbinga kwa ujumla. Mradi huu unatarajiwa kurahisisha usafirishaji wa pembejeo na mazao ya wakulima hususan kahawa na mazao ya nafaka, hivyo kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakazi wa maeneo haya”.
Mhandisi Musa ameongeza kuwa Wilaya ya Mbinga inasimamia mtandao wa barabara wenye urefu wa kilomita 2,037, ambapo kilomita 45 ni za lami, kilomita 207 ni za changarawe na kilomita 1,780 ni za udongo.
“Kutokana na jiografia ya eneo hili kuna zaidi ya madaraja 300.
Awali, bajeti ya wilaya kwa ajili ya barabara ilikuwa shilingi bilioni 1.7, lakini katika kipindi cha Awamu ya Sita bajeti imeongezeka hadi kufikia bilioni 5.2”, ameongeza kusema.
Amesema kwamba ongezeko hilo limewezesha ujenzi wa kilomita 8 za barabara ya lami, ufungaji wa taa mpya 53 na ufunguzi wa zaidi ya kilomita 300 katika halmashauri zote mbili za wilaya hiyo.
Aidha, Mhandisi Musa ameishukuru Serikali kwa ongezeko hilo la bajeti ambalo ni zaidi ya asilimia 200, akisema limechangia kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma kwa wananchi.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, TARURA Mbinga inatarajia kujenga madaraja ya mawe 12, kufanya matengenezo ya barabara za kiwango cha lami kilomita 1.8, kufunga taa za barabarani zipatazo 18 na kufungua barabara mpya kilomita 120 kwa kuweka changarawe katika kilomita 36.
Katika kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi, TARURA wilayani Mbinga imeendesha mafunzo kwa vikundi kazi ambapo jumla ya washiriki 24 walihudhuria na vikundi vinne vimesajiliwa rasmi. Vikundi hivyo tayari vimepata kazi katika awamu tofauti za miradi ya barabara wilayani humo, hatua inayolenga kuongeza ajira na ushiriki wa jamii katika maendeleo ya miundombinu.
Naye, Bw. Theofred Komba, mkazi wa Utili amesema kwamba wanamshukuru Mhe. Rais kwa kuwajali wananchi wake kwani ujenzi wa barabara hiyo utawasaidia kusafirisha mazao yao pia kuwaondolea adha ya usafiri kwani awali walikuwa wakilipa shilingi 5000 lakini kwa sasa wanalipa 3000.
Bi. Leonia Komba mkazi wa Utili amesema kukamilika kwa barabara hiyo itawasaidia wajawazito kufika kwa wakati kwenye kituo cha afya tofauti na zamani ambapo ilikuwa ngumu kuwahi huduma hususan kipindi cha mvua ilikuwa shida sana.

Post A Comment: