Na Joachim Nyambo.

PJT-MMMAAM ni Programu Jumuishi ya Taifa inayolenga kuyaangazia Malezi,Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto(MMMAM) hapa nchini.Ujio wa programu hii unatokana na changamoto nyingi wanazopitia watoto kwenye ukuaji wao hadi kufikia umri ulio timilifu.

Kwa kutambua umuhimu wa mtoto kukuwa kwenye mazingira yaliyo wezeshi kwa ukuaji wenye tija,serikali nchini ilizindu program ya PJT-MMMAM Desemba mwaka juzi jijini Dodoma.Programu ililenga kuleta uchechemuzi kwenye maeneo makuu matano muhimu katika makuzi ya mtoto nayo ni Afya bora,lishe kamili,ulinzi na usalama,malezi yenye mwitikio na ujifunzaji na uchangamshaji wa awali wa mtoto katika umri wa tangu miaka sifuri hadi minane.

Baada ya uzinduzi kitaifa serikali kwa kushirikiana na wadau ukiwemo Mtandao wa malezi,makuzi na maendeleo ya awali ya mtoto(Tecden) iliamua programu kwa matazamio ianze kutekelezwa kwenye mikoa 10 ya awali kabla ya kuenea nchi nzima.Mkoa wa Mbeya ulibahatika kuwa miongoni mwa mikoa hiyo kumi ya awali ambapo uzinduzi kimkoa ulifanyika Agosti 19 mwaka jana ikiwa ni kuonyesha utayari wa mkoa kuanza kuitekeleza kwa mkazo na kwa ushirikishwaji wa wanajamii na wadau wote mkoani hupa.

Tayari sasa ni robo mbili za utekelezaji wa vipindi vya miezi mitatu mitatu imetiamia.Wadau wanakiri matokeo chanya yameanza kuonekana kwa afua mbalimbali zinazohusiana na watoto wadogo kuonekana kutekelezwa kwa mkazo zaidi ya awali kabla ya ujio wa programu.

Baadhi ya matokeo chanya ya PJT-MMMAM yalibainishwa kwenye kikao kazi maalumu cha Tathmini ya Robo ya pili ya utekelezaji wa programu husika kilichofanyika hivi karibuni.Baadhi ya matokeo yanaonesha kuwafurahisha wadau wengi mkoani hapa hasa wanapoaanza kuona sasa nguvu kubwa inaanza kuwekezwa kwenye kundi la watoto.

Miongoni mwa matokeo chanya yanayoonekana ni pamoja na halmashauri kuanza kushirikiana kwa karibu na kuwa na takwimu za pamoja za shughuli zinazofanywa kwenye maeneo yao hatua inayowezaesha kuwa na uelewa wa pamoja juu ya watoto.Watoto walio na umri wa chini ya miaka nane wanapewa kipaumbele na program hii kwakuwa wako kwenye umri muhimu wa ukuaji wa ubongo.

Mfano mzuri ni katika Wilaya ya Chunya ambapo ilielezwa miongoni mwa mafanikio chanya ya PJT-MMMAM ni pamoja na ongezeko la wazazi na walezi waliopewa elimu ya Lishe bora na Unyonyeshaji watoto.

Afisa Maendeleo ya Jamii wilayani humo,Nasra Mkupete anasema hadi Januari Mwaka huu wazazi na walezi 39,567 walikuwa wamepewa elimu ya lishe bora na unyonyeshaji.

Mkupete anasema miongoni mwa watu waliopewa kipaumbele kwenye utoaji wa elimu ya lishe bora na unyonyeshaji ni pamoja na wanawake wajawazito pamoja na wenza wao ili kuimarisha usimamizi sahihi wa milo kwenye kaya zao

Anasema kupitia utoaji huo wa elimu pia kumekuwepo na mafanikio makubwa ya utoaji wa madini chuma na dawa za minyoo kwa kufikia asilimia 94.9 ambapo awali malengo yalikuwa kuwafikia wajawazito 17,236 na hadi kufikia Januari walifikiwa 16,360.

Kwa upande wa utoaji wa matone ya Vitamini A  watoto 45,102 sawa na asilimia 105 walipata huduma hiyo na kuwezesha kuvuka malengo waliyokuwa wamejiwekea awali.

“Siku ya Afya na Lishe ya Kijiji lengo lilikuwa kuwafikia watoto 43,679 lakini tumefanikiwa kufikia watoto 39,243 ambao ni sawa na asilimia 90.Kwa watoto waliofikiwa na kutambuliwa hali zao ni 10,989 sawa na asilimia 28 ni watoto walio duma,watoto 4,512 sawa na asilimia 11.5 ni watoto wenye utapiamlo wa kadri na watoto 29 sawa na asilimia 0.1 wana utapiamlo mkali.” Alisema afisa huyo.

Akizungumzia malezi yenye mwitikio Mkupete alisema elimu ya malezi na makuzi ya watoto imetolewa kwa watoa huduma ngazi ya jamii 34 katika vijiji saba  kwa kushirikiana na Shirika la Sharom na CRS.

Atuganile Mbelwa ni afisa maendeleo ya jamii kutoka halmashauri ya Wilaya ya Kyela,akimwakilisha Afisa maendeleo ya jamii wa wilaya hiyo alisema miongoni mwa shughuli zilizofanyika kwenye robo hiyo ni pamoja na kutoa elimu kwa viongozi wa dini na wanahabari juu ya masuala ya malezi na makuzi ya mtoto.

“Malengo yetu ilikuwa kutoa elimu kwa waandishi wa habari nane lakini tukafanikiwa kutoa kwa wanne halmashauri ikiwa imetenga bajeti ya Shilingi 320,000 tukawafikia.Kwa viongozi wa dini tuliwafikia 20.”

“Kwenye hii robo ya pili pia tulifanya mikutano mitatu ambapo halmashauri ilitenga Shilingi milioni 1.5.Kwa sasa vituo vya MMMAM vipo 44 japo hivi tulivibaini awamu ya nyuma kwa kupitia Shirika la Tumaini lililotenga Shilingi laki 4.5.”anasema Mbelwa.

Afisa huyo anasema kwenye robo ya pili kupitia bajeti ya halmashauri iliyotenga kiasi cha Shilingi milioni 2.5 waliweza kuzifikia kaya zinazonufaika na Mpango wa serikali ya kunusuru kaya masikini kupitia Tasaf kwenye vijiji 19 na kutambua jumla ya watoto 128 walio na umri wa chini ya miaka nane.

Leah Mwakajobe ni Afisa Ustawi wa Jamii kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Wanawake na Makundi maalumu.Anautaja Mkoa wa Mbeya kuwa miongoni mwa mikoa inayofanya vizuri kwenye utekelezaji wa PJT-MMMAM.

Mwakajobe alisema kufanyika kwa vikao vya tathimni katika kila robo ya mwaka ya utekelezaji ni sehemu ya maagizo yanayotakiwa kufanyiwa kazi na mikoa yote iliyokwishaanza kutekeleza programu hiyo.Hiyo ndiyo inatoa sura ya nini kinachofanyika na upi mwelekeo wa utekelezaji kwa mkoa husika.

“Vikao hivi ni muhimu na ni matakwa ya Serikali kupitia programu yenyewe ya PJT-MMMAM.Niwapongeze Mbeya kwa kufanya vikao hivi kwa kuzingatia miongozo.Tunaona pia wanazingatia yale mambo matano yanayotekelezwa na programu husika.”

“Mbeya wamefanya vizuri katika utekelezaji wa mradi kwa kuzingatia afua ambazo zipo katika program nay ale mambo makuu matano.Kwa mfano kwenye kipengele cha malezi changamshi kwa watoto,namna walivyofanya shughuli za ulinzi na usalama kwa watoto,masuala ya afya na lishe.”

Pamoja na mwamko mkubwa kwenye utekelezaji wa program hii,changamoto ya baadhi ya halmashauri kutotenga bajeti inatajwa kukwamisha baadhi ya shughuli.Hii inasababisha wizara kutoa msukumo kwa halmashauri zote kuhakikisha kwenye bajeti zao hazisahau afua muhimu za programu husika.

Kwa mujibu wa Mwakajobe bado kuna baadhi ya halmashauri zinasuasua kwenye utengaji bajeti kwaajili ya utekelezaji wa shughuli za programu hii hatua inayoweza kukwamisha nia ya serikali pamoja na wadau walioona umuhimu wa kuitekeleza ukiwemo Mtandao wa Malezi na Makuzi ya Awali ya mtoto nchini (Tecden).

Anasema halmashauri kwa kushirikiana na wadau waliopo kwenye maeneo yao zinapaswa kuona umuhimu wa kutenga bajeti ili yanapokuja kushindanishwa matokeo ya utekelezaji ya programu husika kila eneo lijipime kwa kile kilichofanyika.

“Tunasisitiza halmashauri kutenga bajeti kwaajili ya hizi shughuli.Kama usipoweka mpango wa bajeti ina maana kile kitu hutoweza kukitekeleza lakini kama kwa mwaka huu ukatenga bajeti hata kama ni kidogo ina maana kwa kiasi flani utaweza kutekeleza..ina maana ukiendelea hivyo hata miaka inayofuata utaendelea kukitekeleza.” Alisisitiza Mwakajobe.

Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii mkoa wa Mbeya,Aika Temu anasema kwa halmashauri kuanza kujiweka kwenye mlengo wa kutenga bajeti kwaajili ya MMMAM utekelezaji wa shughuli za programu hiyo zitakuwa endelevu hata baada ya mfadhili kuondoka.

“Tunashukuru tunaona kuna halmashauri ambazo kidogo zimekwishaanza kutenga bajeti kutoka kwenye mapato yao ya ndani kwaajili ya shughuli hizi.Kwetu sisi hii ni hatua kubwa.” Alisema Temu.

Selina Mtenya ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Mbeya,anasema tayari kama wataalamu ngazi ya mkoa wameanza kuchukua hatua kwa halmashauri zinazoonekana kuleta legelege kwenye kutenga bajeti ya shughuli za programu hii.

“Sisi kama mwataalamu katika ngazi ya Mkoa lazima tufanye ufuatiliaji mfano tumetoka kwenye kipindi cha kufanya maandalizi ya bajeti  na bajeti za halmashauri  kabla ya kutumwa wizarani lazima zipite ofisi ya Mkuu wa Mkoa,kupitia zile bajeti tulikuwa tunakagua  ni halmashauri zipi ambazo hazikuingiza  bajeti za PJT-MMMAM kwenye mpango wao.”

“Kuna baadhi ya halmashauri walikuwa wakituma bajeti zao tulipokagua tukaona hazikuweka hizo bajeti tulikuwa tunawarudishia  kwamba tunaomba muongeze na shughuli za MMMAM.” anasema Mtenya.

Share To:

Post A Comment: