Na John Walter-Manyara

Wanawake nchini wametakiwa kuvunja ukimya juu ya ukatili wanaofanyiwa na badala yake watoe taarifa polisi ili hatua zichukuliwe kwa wahusika kukomesha vitendo hivyo.

Hayo yameelezwa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya Wanawake duniani na Kamanda wa polisi mkoa wa Manyara George Katabazi yaliyofanyika katika kijiji cha Mamire wilayani Babati.

Kamanda amewataka wanawake hao kuvunja ukimya kwa kuripoti katika madawati ya jinsia vituo vya polisi kwani  matukio mengi ya mauaji yanatokea kwa kukaa kimya muda mrefu  kuvumilia vipigo.

Ameitaka halmashauri ya wilaya ya Babati na wadau mbalimbali kuziimarisha kamati zilizoundwa kwa ajili ya kutokomeza vitendo vya ukatili kwani mkoa wa Manyara hali sio nzuri.

Katika hatua nyingine kamanda Katabazi ameshauri wanawake na wanaume kuwa na matumizi sahihi ya mitandao ya kijamii na kuacha kufuatilia simu za wapenzi wao kwa kuwa ni kisababishi cha migogoro na mauaji ya wivu wa mapenzi.

Katika taarifa iliyosomwa na mkuu wa idara ya Maendeleo ya jamii Halmashauri ya wilaya ya Babati Januari Bikuba, wameendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo kuweka mazingira wezeshi kwa watoto wote wakiwemo wa kike kwa kuchukua hatua mbalimbali za kupambana na ukatili wa aina hiyo.

Hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mabaraza ya watoto ambapo jumla ya mabaraza 25 katika ngazi za kata na mabaraza 40 ya ngazi za vijiji, yamehuishwa na kupatiwa mafunzo juu ya haki za watoto, wajibu wao na stadi za maisha pamoja na kuunda kamati za kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambapo jumla ya kamati 25 zimeundwa kwa ngazi za kata, na kati ya hizo 15 zimejengewa uwezo kuhusu uongozi na majukumu yao, kwa ngazi ya vijiji zipo kamati 102 huku 50 zikijengewa uwezo kwa kupatiwa mafunzo.

Taarifa ya Bikuba imeeleza Halmashauri ya wilaya ya Babati katika kutomeza vitendo vya ukatili wa kijinsia imeunda kamati za ulinzi na utetezi  kwa mtoto katika kata zote 25 za Halmashauri hiyo.

Mwenyekiti wa Mtandao wa Polisi Wanawake Tanzania (TPF- Net) mkoa wa Manyara (RTO) ASP Georgina Matagi amesema kila mtanzania mwenye akili timamu ana haki ya kumlinda mtoto wa kike na wa kiume na kuondoa dhana iliyokuwa zamani kuwa mwanamke hawezi.

Amesema kwa sasa watoto wanaoathirika Zaidi ni wa kiume akitolea mfano wimbi lililopo kwa sasa la ulawiti na mapenzi ya jinsia moja.

KAULI MBIU’ Ubunifu na mabadiliko ya kiteknolojia, chachu katika kuleta usawa wa kijinsia’.

Share To:

Post A Comment: