Naibu Waziri wa Kilimo Anthony Mavunde amewataka wafanyakazi wapya 320 walioajiriwa hivi karibuni kwenda kusimamia miradi ya umwagiliaji kikamilifu katika wilaya watakazopangiwa ili miradi hiyo ilete tija na kuboresha hali za wakulima nchini Tanzania.

Naibu Waziri Mavunde ameyasema hayo  Jijini Dodoma alipokuwa akizungumza na wafanyakazi hao katika semina ya siku tatu ya mafunzo ya usimamizi wa miradi ya umwagiliaji kabla hawapangiwa vituo vyao vya kazi.

“Ni dhahiri kila mmoja wenu ameiona dhamira njema ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kukuza sekta ya kilimo hapa nchini kupitia umwagiliaji kwa kuiongezea bajeti Tume ya Umwagiliaji kufikia Bilioni 361.

Nendeni mkasimamie miradi hii ya umwagiliaji kwa uadilifu na weledi mkubwa ili iweze kuleta matokeo chanya kwenye ukuaji wa sekta ya kilimo na kufikia malengo ya kukikuza kilimo kwa asilimia 10 ifikapo mwaka 2030.

Ninyi bahati nzuri wengi ni vijana chini ya miaka 35 mmeaminiwa na serikali kwenda kuzifanya kazi hizi,itunzeni hii imani kwa maslahi mapana ya Taifa Tanzania ili mwisho wa siku mkulima wa Tanzania anufaike na ujuzi na maarifa yenu.

Mkisimamia miradi hii vyema kwa uweledi na uzalendo,watakaonufaika ni wakulima wa Tanzania ambao pia wataongeza uzalishaji na kuifanya sekta ya kilimo

Kuendelea kuchangia kwa kiwango kikubwa kwenye pato la Taifa”Alisema Mavunde

Akitoa maelezo ya awali Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Ndg. Raymond Mndolwa amesema mafunzo hayo kwa waajiriwa wapya ni mahsusi katika kuwajengea uwezo kwenda kusimamia miradi ya umwagiliaji nchini kote ili iweze kuleta matokeo chanya katika kuikuza sekta ya kilimo.

Share To:

Post A Comment: