Na. Majid Abdulkarim, Tabora


Serikali kupitia Wizara ya Afya imewataka Waganga wakuu wa Mikoa na Halmashauri nchini kuhakikisha watoto wote chini ya miaka mitano katika maeneo yao wanapatiwa chanjo ili kuepuka magonjwa ya milipuko. 

Agizo hilo limetolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Dkt. Grace Magembe leo Mkoani Tabora wakati alipofanya ziara katika kituo cha afya Maili Tano na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete Tabora kwa lengo la kujionea hali ya utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.

Dkt. Grace amewataka wataalamu wa afya kila wanapo kwenda kufanya huduma za mkoba lazima na huduma ya utoaji chanjo iwepo  ili kuongeza kasi katika utoaji chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano.

“Kuna watoto 48,000 mkoani Tabora hawajafikiwa kupatiwa chanjo na wengine wamepata nusu dozi ya chanjo, hivyo ni wajibu wetu kuwafikia na kuhakikisha tunawapatia chanjo ili kuokoa maisha yao”, ameeleza Dkt. Grace

Amesema kuwa haoni haja ya kuona watoto wanapoteza maisha wakati chanjo zipo za kuongeza kinga ili kuwaokoa wasipoteze maisha yao kwani watoto ni taifa la kesho.

Hivyo Dkt. Grace amesisitiza wataalamu wa afya kutoa elimu kwa jamii juu ya umuhimu wa chanjo kwa watoto chini ya miaka mitano pamoja na matumizi sahihi ya kadi ya kliniki ya mtoto .

Pia ,amewataka kuongeza kasi ya uchanjaji katika maeneo yao ili kuepukana magonjwa ya mlipuko kama vile surua na magonjwa mangine ambayo yanazuilika kwa kuwapatia chanjo watoto waliopo chini ya miaka mitano

Katika Hatua nyingine  Dkt. Grace ametoa pongezi kwa watumishi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa Kitete Tabora pamoja na watumishi wa kituo cha afya cha Maili Tano kwa kazi nzuri wanazofanya ya kuwatumikia Watanzania katika kutoa Huduma za afya

Vile vile Dkt. Grace amepata nafsi ya kuongea na wananchi waliofata huduma katika hospitali ya ya Rufaa ya Mkoa Kitete na kuwasisitiza wananchi hao kujiunga na Bima ya afya ili kujihakikishia uhakika wa matibabu pale wanapo ugua.

Dkt Grace amewasisitiza Wananchi waliojitokeza kupata huduma katika hospital ya Rufaa ya mkoa Kitete TABORA kujiunga na bima ya afya ili kuwa na wakika wa matibabu  wakati wanapo ugua

Akizungumza Dkt. Grace amempongeza Mtumishi wa Mlinzi wa Wodi ya Wazazi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Kitete Tabora,  Bi. Hamida Iddy Fundi kwa kufanya vizuri katika swala zima la huduma kwa mteja.

“Huyu kasemewa na wananchi wanao kuja kufata huduma hapa kuwa analugha nzuri, anaukarim kila mteja anapofika kupata huduma katika hospitali hii anazungumza naye kwa ukarimu “, ameeleza Dkt. Grace

Katika hatua nyingine amewakumbusha watumishi wote kuwa makini kila wanapotoa huduma za afya kwa lengo la kulinda usalama wa afya zao pamoja na mgonjwa anayehudumiwa.

Share To:

Post A Comment: