Na. Angela Msimbira OR-TAMISEMI


Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  Dkt. Philip Mpango, amewaonya watendaji wa kata kuacha kuwa  miungu  watu kwa kuwakamata wananchi na kukamata mali zao kwa uonevu bila kufuata  Sheria, Kanuni na Taratibu za kazi.


Ameyasema hayo leo  tarehe 14 Februari, 2023 Jijini Dodoma kwenye hafla ya kukabidhi magari kwa Mameneja wa Mikoa na Wilaya wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini(TARURA) na pikipiki kwa watendaji wa kata.


Amesema kuwa kumekuwemo na malalamiko kuhusu ukiukwaji wa maadili ya uongozi wa umma unaofanywa na Watendaji wa Kata hivyo amewataka kuhakikisha wanasimamia Sheria bila kuonea wananchi


“Msijifanye miungu watu kwa kuwakamata wananchi na kupora mali zao kwa uonevu, simamieni sheria lakini msionee watu, sisi huku juu tunaletewa tuhuma nyingi za ukiukwaji wa maadili ya viongozi wa umma ambazo zinafanywa na baadhi yenu Maofisa Watendaji wa Kata,”amesema 


Dkt. Mpango amewataka Watendaji wa Kata wote nchini kuhakikisha wanafanyakazi kwa weledi, uaminifu kwa kuwa ndio kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi.


Amewataka Wakurugenzi wote nchini kufuatilia tuhuma hizo na kuchukua hatua stahiki za kisheria na kinidhamu.


Ameeleza  kuwa kazi ya Mtendaji wa  Kata ni kumsaidia Mkurugenzi wa Halmashauri katika kusimamia shughuli za maendeleo katika kata zao, hivyo amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri  kuhakikisha wanawasimamia Watendaji wa Kata katika kutekeleza majukumu yao yakiwemo ufanyikaji wa vikao na mikutano ya Kisheria.


Kuhusu ugawaji wa Pikipiki Dkt. Mpango amewaagiza Wakurugenzi wa Halmashauri kuhakikisha wanagawa pikipiki hizo kwenye kata zilizopo pembezoni na kata zenye maeneo makubwa ili kuweza kuwafikia wananchi kwa urahisi.


Naye, Waziri wa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Mhe. Angellah Kairuki, amesema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan alikubali pendekezo la kutumika Sh.Bilioni 2.9 za mgao wa kodi ya majengo kuanzia Julai, 2021 hadi Februari, 2022 ili kununua vitendea kazi hivyo kwa watendaji wa kata.


Aidha, amesema pikipiki hizo zitaongeza idadi ya watendaji wenye vitendea kazi hivyo kuwa zaidi ya 1,500 kati ya kata 3,956 zilizopo.

Share To:

Post A Comment: